“When I see an anxious person, I ask myself, what do they want? For if a person wasn’t wanting something outside of their own control, why would they be stricken by anxiety?”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 2.13.1
Tumepata nafasi nyingine nzuri ya kuiona siku hii mpya kwetu rafiki.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari CHANZO CHA WASIWASI…
Chanzo kikuu cha wasiwasi kwenye maisha yako ni kutaka kitu ambacho kipo nje ya uwezo wako.
Pale unapotaka kitu kiende kama unavyotaka wewe, wakati kitu hicho kipo nje ya uwezo wako, ndiyo unazalisha wasiwasi.
Wasiwasi na hata hofu ni kitu cha kujitakia mwenyewe.
Ni pale unapotaka kila mtu afanye kama unavyotaka wewe, wakati huna udhibiti juu yao.
Ni pale unapokuwa umechelewa mahali na ukakutana na foleni halafu ukataka foleni iende haraka ili iwahi, wakati foleni hiyo haipo kwenye udhibiti wako.
Kila unapojikuta kwenye fikra za kutaka kitu kiwe kama unavyotaka wewe, wakati kitu hicho kipo nje ya uwezo wako, jua unazalisha wasiwasi na hofu ambayo huna cha kufanya ili kuiondoa.
Njia bora ya kuondokana na wasiwasi na hofu hizi tunazozalisha ni kujiuliza juu ya kila unachotaka, je kipo ndani ya uwezo wako?
Kama kitu kipo nje ya uwezo wako achana nacho, maana utajijaza wasiwasi ambao huwezi kuufanyia chochote.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutaka yale yaliyopo ndani ya uwezo wako na kupokea yaliyo nje ya uwezo wako kama yanavyokuja kwako.
#WasiwasiMzigo, #TakaUnachodhibiti, #DuniaHaiendiKwaMatakwaYako
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha