Ukuaji umekuwa kikwazo cha mafanikio ya wengi.

Wengi wamekuwa wanaanza na malengo makubwa na kuweka juhudi kubwa mwanzoni, lakini wanafika mahali ambapo wanafanya kwa mazoea na hakuna ukuaji tena. Hapa ndipo wengi wanapokwama na kuwa na maisha ya mazoea huku wakipata matokeo ambayo wamezoea kupata.

Hapa ndipo mtu anapokuwa kwenye kazi ile ile kwa zaidi ya miaka kumi lakini hapigi hatua, au anakuwa kwenye biashara ile ile kwa miaka mingi na hakuna hatua za ziada anazopiga.

Kudumaa kwa ukuaji kumekuwa kunatokea kwenye mahusiano pia, mtu anakuwa kwenye mahusiano ambayo hayakui, yako vile vile kila wakati na yanamchosha.

Ukuaji ndiyo msingi mkuu wa mafanikio, bila ya ukuaji hakuna mafanikio. Hivyo hili ni muhimu sana kulizingatia, kwenye kila unachofanya hakikisha kila siku unakua zaidi, kila siku unapiga hatua mpya na siyo kwenda tu na mazoea.

Sasa watu wengi wamekuwa hawajui ukuaji wa kimafanikio ni nini hasa. Wengi hufikiri labda kujaribu kitu kipya ndiyo kukua. Lakini huo siyo ukuaji halisi.

Zipo dalili tatu muhimu za kupima ukuaji wako kwenye chochote unachofanya na zinaashiria kwamba unaelekea kwenye mafanikio makubwa.

Moja; unakataa vitu ambavyo awali ulikuwa unavikubali. Watu wengi huendelea kung’ang’ana na vitu kwa sababu tu walishavikubali awali. Kama unaendelea na kukubaliana na vitu ulivyokubali awali kwa sababu tu ulishavikubali basi hakuna ukuaji hapo. Unapoanza kuona unakataa vitu ambavyo awali ulivikubali, jua kuna ukuaji unaendelea ndani yako.

Mbili; unaachana na vitu ambavyo umekuwa unavitegemea. Hiki ni kipimo muhimu kwa sababu wengi wakishapata kitu ambacho wanakitegemea, basi hutegemea hicho maisha yao yote. Hawathubutu kuachana nacho kwa sababu wanahofia hawawezi kupata kingine wanachoweza kutegemea. Ukishaona upo tayari kuachana na kitu ambacho umekuwa unakitegemea sana, jua hapo unakua.

Tatu; unaacha kufanya vitu ambavyo havileti matokeo unayotaka. Kuna vitu vingi ambavyo huwa tunaanza kufanya, lakini baadaye tunagundua havileti yale matokeo ambayo tulikuwa tunayategemea. Pamoja na kugundua vitu hivyo havileti matokeo tunayotaka, wengi huwa hawana ujasiri wa kuviacha. Wengi huendelea kufanya kwa sababu walishaanza au walishawaahidi watu kitu. Ukiona unaweza kuacha kufanya kitu ambacho hakileti matokeo unayotaka, hata kama ulishawaahidi watu, basi hapo unakua.

Rafiki, umeona vipimo hivyo vitatu, siyo rahisi na ni vigumu sana kwenye maisha yetu ya kawaida, na ndiyo maana wengi hawakui, kwa sababu hawathubutu kuchukua hatua hizo za ukuaji.

Mfano mzuri wa kuogopa ukuaji kwa wengi ni kuacha kazi inayolipa na kwenda kuanzisha biashara, wengi huwa wanahofia sana kuacha ajira na kwenda kwenye biashara, na hilo linawafanya wabaki pale pale miaka yao yote. Kuacha kile ulichozoea hata kama kinalipa vizuri na kufanya kile ambacho ni bora zaidi ni hitaji kubwa sana kwenye ukuaji.

Angalia namna ya kuchukua hatua hizi tatu kwenye kila eneo la maisha yako na utaweza kukua zaidi ya hapo ulipo sasa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha