“Whenever you get an impression of some pleasure, as with any impression, guard yourself from being carried away by it, let it await your action, give yourself a pause. After that, bring to mind both times, first when you have enjoyed the pleasure and later when you will regret it and hate yourself. Then compare to those the joy and satisfaction you’d feel for abstaining altogether. However, if a seemingly appropriate time arises to act on it, don’t be overcome by its comfort, pleasantness, and allure—but against all of this, how much better the consciousness of conquering it.”
—EPICTETUS, ENCHIRIDION, 34
Siku mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi nyingine nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari RAHA INAWEZA KUWA ADHABU…
Kuna mambo mengi ambayo tunapata msukumo na tamaa ya kuyafanya kwa sababu tunajua tukiyafanya tutapata raha.
Lakini kwa kufanya mambo hayo, tunapata raha kidogo, lakini mwishowe raha hiyo inaishia kuwa adhabu kubwa kwetu.
Na hii ndiyo changamoto kubwa sana kwenye raha, kila chenye kuleta raha, kinakuja na adhabu yake.
Utumiaji wa vilevi unaleta raha kwa muda mfupi, lakini kadiri mtu unavyoendelea kutumia ndivyo inavyokuwa adhabu kubwa kwako. Pale unapokuwa umelewa hupati raha tena bali maumivu. Mwili unachoka na kuuma kila mahali kwa sumu ya kilevi kilicholeta raha ya muda mfupi.
Kadhalika kwenye raha ya ulaji, ufanyaji wa mapenzi, kuzurura mitandaoni na mengine tunayosukumwa kufanya ili tu kupata raha.
Kama anavyotuambia Mstoa Epictetus, tunapaswa kujilinda sana na raha tunazokimbilia ili zisije kuwa maumivu kwetu.
Anatuambia kabla hayujakimbilia raha, tuwe na subira kwanza na tufikirie pande zote mbili, moja pale tunapokuwa tumefurahia kitu hicho na mbili pale ambapo tunakijutia.
Kisha tulinganishe majuto na maumivu tutakayopata na raha tutakayopata kwa kuacha kufanya hicho kinacholeta raha ya muda mfupi.
Maisha bora yanahitaji sana mtu kujidhibiti wewe mwenyewe, kwa sababu jamii haiwezi kujidhibiti na waka kukudhibiti. Watu wengi kwenye jamii wamepotea kwa sababu kikubwa wanachofanya ni kukimbiza kila aina ya raha na mwisho wanaishia kwenye maumivu.
Usiwe mmoja wa hao ambao wanakimbizana na raha zinazokuwa adhabu kwao.
Tafakari kabla hujafanya kile unachosukumwa kufanya kwa ajili ya raha, jiulize baada ya raha hiyo nini kinakuja? Ukishapata jibu, chukua hatua sahihi.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuepuka raha kuwa maumivu na adhabu kwako.
#RahaAdhabu, #TafakariKablaYaKufanya, #DhibitiHisiaZako
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha