Mpendwa rafiki,

Kila mtu anapenda familia yake iwe na furaha lakini siyo kila familia ina furaha. Familia ndiyo msingi wa mambo yote hapa duniani. Kama ni viongozi wa zuri basi tunawapata katika familia na watu bora tunawapata kutoka katika familia bora.

Matunda mazuri tunayoona au tunayapata katika jamii zetu ni matokeo ya familia bora. Ili tuwe na jamii bora tunapaswa kwanza kuwa na familia bora. Kila familia inapaswa kujenga misingi bora ili tuweze kuwa na jamii bora.

Familia nyingi za sasa hazina misingi bora, zinaishi tu kimazoea hivyo siyo rahisi kukuta familia zetu za sasa zinaishi katika misingi bora au falsafa fulani.

Kuna mambo ya ajabu ambayo yanaendelea katika familia zetu na kama tukisema tuzifunue yale ya ndani ya familia zetu , basi ni aibu tupu, hakuna familia ambayo iko salama kwa kila kitu.

Familia ambayo haina furaha, ni familia ambayo imekosa upendo. Familia ambayo haina upendo haiwezi kuwa na furaha. Katika upendo tunapata yote ndani ya familia. Upendo ndiyo mama wa mafanikio ya kila familia na kama tunataka kupata familia bora basi tuwekeze katika familia zetu kuhakikisha tunajenga misingi ya upendo.

malezi bora
silhouette of parents and their children on the beach

Misingi ya upendo ikiwepo katika familia tutaweza kuwa na furaha. Angalia familia ambazo hazina furaha utagundua hazina upendo. Nioneshe familia yenye upendo ambayo haina furaha jibu ni kwamba hakuna.

SOMA; Imani Saba (7) Potofu Zinazokuzuia Usiwe Tajiri Kwenye Maisha Yako Na Jinsi Ya Kuzivuka.

Katika kujenga misingi ya upendo katika familia tunapaswa kuzingatia haya kwanza;

Upendo unatakiwa uanze na kila mwanafamilia kujipenda yeye mwenyewe. kila mwanafamilia akiweza kujipenda yenye mwenyewe ataweza kumpenda hata mwenzake.

Ni uongo kusema unampenda mwenzako katika familia wakati wewe mwenyewe hujipendi. Hivyo upendo uanze na kujipenda na sisi wenyewe.

Pili, tuwapende na wengine. unaweza kusema unampenda mwingine kama wewe mwenyewe unajipenda. Tukiishi kwa falsafa hii ya kuwapenda wengine na kujipenda wenyewe lazima kila mmoja atajali maslahi ya mwingine hivyo familia lazima iwe na furaha.

Tatu, katika familia zetu tunapaswa pia kuzipenda na kupenda yale kile wanachofanya familia. Kuna watu wengine hawazipendi familia zao wala kile wanachofanya kama mtu hupendi kile wanachofanya familia yako huwezi kuwa na furaha. Unaweza kubadilisha marafiki lakini huwezi kubadilisha familia hivyo katika familia tunapaswa kuvumiliana na kusaidiana. Kila mmoja awe msaada kwa mwingine, tubebeane mizigo.

Hatuwezi kuwa sawa katika familia zetu hata siku moja. Ila tunaweza kuishi maisha ya upendo na upendo ukaziba yale yote ambayo yanaonekana vibaya. Kuna nguvu kubwa sana kwenye upendo hivyo mimi na wewe tujaribu kuweka misingi ya upendo na tutakuwa na familia bora sana.

SOMA; Jukumu Kubwa La Mzazi Katika Familia

Hatua ya kuchukua leo; jenga familia yenye upendo na furaha itakuja yenyewe. Upendo unapenda kukaa mahali penye amani na ushirikiano hivyo jitahidi kufanya yale ambayo familia inadai na siyo vinginevyo.

Kwahiyo, kama unataka familia yako ifanikiwe anza kwanza kufanikiwa wewe, jibadilishe vile ambavyo unataka familia yako iwe na familia yako itakuwa. Ni uongo kutaka wengine wabadilike wakati wewe hutaki kubadilika.

Makala hii imeandikwa na

Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net

Asante sana