Rafiki, eneo kubwa tunalokwama katika kupiga hatua kwenye maisha ni aina ya maamuzi ambayo tunafanya. Kwa kuwa maamuzi ndiyo yanayoamua ni hatua zipi tunachukua, tukifanya maamuzi bora tutachukua hatua kubwa na tukifanya maamuzi mabovu tutachukua hatua ambazo siyo nzuri.
Kuna mitazamo miwili ya kufanya maamuzi ambayo unapaswa kuijua na kujua mtazamo ulio sahihi kwako.
Mtazamo wa AMA/AU.
Kumbuka maamuzi huwa yanakuwa magumu kufanya pale unapokuwa na vitu zaidi ya kimoja unavyopaswa kufanya na hujui uchague kipi. Hapa ndipo unapoingia kwenye mtazamo wa AMA/AU. Hapa unajiuliza ufanye kipi kati ya vile vingi vya kufanya vilivyojitokeza. Kuna wakati mtu unaweza kuwa njia panda na ukashindwa kabisa kufanya maamuzi, ukabaki unajiuliza nifanye hiki AMA kile, nifanye hivi au vile. Mtazamo huu huleta msongo na wengi hukwama wasijue hatua ipi ya kuchukua.
Mtazamo wa PAMOJA/NA.
Huu ni mtazamo wa kuwa tayari kufanya vyote kwa pamoja. Unapokuwa na zaidi ya kitu kimoja cha kufanya, badala ya kukaa kwenye njia ya panda ufanye kipi na uache kipi, unachagua kufanya vyote kwa pamoja. Mtazamo huu siyo tu unakuondolea msongo, bali pia unakupa wigo mpana wa vitu unavyoweza kufanya na hata kukupa fursa kubwa ya kufanikiwa. Ukiwa tayari kufanya yale yanayokuweka njia panda, hakuna kinachoweza kukuzuia kufanikiwa.
Hivyo kuanzia sasa, chagua mtazamo wa PAMOJA/NA katika kufanya maamuzi. Kama unajiuliza uajiriwe AMA ufanye biashara, nenda kwenye mtazamo wa uajiriwe PAMOJA na kufanya biashara.
Najua unaweza kuwa unajiambia huna muda au uwezo w akufanya vitu vingi kwa pamoja, lakini unajidanganya tu au kujifariji, inapokuwa muhimu kweli muda na uwezo vinapatikana. Kwa sababu tayari hivyo vitu unavyo sasa, ila kwa kuwa huvihitaji sana unavipoteza. Utakapoanza kuvihitaji kweli, utaviona jinsi ambavyo unavyo kwa wingi.
Kila unapokuwa njia panda, amua kufanya PAMOJA na hutapoteza muda wako kwenye kusumbuka, badala yake utaupeleka muda na nguvu kwenye kufanya, kitu ambacho kitakuwezesha kupiga hatua zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,