Mara nyingi huwa tunajipa majibu ya vitu ambavyo siyo sahihi.
Mtu unakuwa hujui kitu fulani, kuhusu mtu au jambo, lakini unaamua kujipa majibu wewe mwenyewe, ambayo huwa siyo sahihi, bali ni matokeo ya fikra ulizonazo.
Kwa njia hii tumekuwa tunajidanganya sana sisi wenyewe, tumekuwa tunajipa majibu ambayo siyo sahihi.
Kwa mfano unamsalimia mtu halafu hakuitika, kwa haraka utajiambia mtu huyo ana dharau, huenda utaanza kufikiria mambo gani mliyokosana siku za nyuma. Lakini huenda ungeuliza kwa nini hakuitika, huenda hata hakusikia.
Mara nyingi majibu ambayo tumekuwa tunajipa siyo tu kwamba hayapo sahihi, bali pia yanaegemea upande wa ubaya. Mara nyingi majibu tunayojipa sisi wenyewe yanaegemea upande mbaya wa jambo.
Tunapaswa kuondokana kabisa na hali hii ya kujipa majibu kwa mambo ambayo hatuyaelewi au kuwa na uhakika nao. Kama kuna kitu ambacho hujui, huelewi au huna uhakika nacho, chukua hatua ya kumuuliza mhusika. Mara zote utapata majibu tofauti kabisa na yake ambayo ulikuwa unajipa wewe mwenyewe.
Hupotezi chochote kwa kuuliza, hivyo popote unapokuwa huna uhakika, uliza, itakusaidia sana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,