Rafiki yangu mpendwa,

Maisha yetu ni mjumuiko wa maeneo mbalimbali yanayohusu maisha haya. Hivyo ili kuwa na mafanikio ya kweli kwenye maisha, lazima kuwe na mlinganyo katika mafanikio tunayopata kwenye kila eneo.

Watu wengi wanaokazana kufanikiwa wamekuwa hawapati mafanikio ya kweli kwa sababu huweka juhudi kwenye eneo moja au machache ya maisha na kusahau maeneo mengine.

Kwa mfano mtu anaweza kuweka juhudi sana kwenye kazi yake au biashara yake, na ikamwezesha kuwa na kipato kikubwa sana, lakini akasahau kujenga mahusiano yake au familia yake. Pamoja na kuwa na fedha nyingi, maisha yake yanakuwa hayajakamilika kwa sababu maeneo mengine yanakuwa yameanguka.

Kadhalika mtu anaweza kuweka nguvu kubwa kwenye kujenga mahusiano yake na wengine, akawa na mahusiano bora sana, lakini fedha ikawa changamoto kubwa kwake, akawa kwenye madeni makubwa ambayo yanamkosesha uhuru wa maisha. Licha ya kuwa na mahusiano bora kwa mwenza wake, marafiki na hata familia, anakosa kuyafurahia maisha kila anapofikiria changamoto za kifedha alizonazo.

Katika juma hili la 12 la mwaka 2019, tunakwenda kujifunza kwa kina kutoka kitabu kinachoitwa

The Code of the Extraordinary Mind: 10 Unconventional Laws to Redefine Your Life and Succeed On Your Own Terms ambacho kimeandikwa na Vishen Lakhiani.

Katika kitabu hiki, Vishen anatuonesha jinsi ambavyo wale waliofanikiwa sana wanafikiri tofauti na watu wa kawaida na wanayatengeneza maisha wanayotaka wao na siyo kuishi maisha ya kuiga na ya mazoea, yale ya kufanya kile ambacho kila mtu anafanya. Katika makala ya tano za juma hili nitakushirikisha kwa kina kanuni kumi za kuishi maisha yasiyo ya kawaida.

Lakini katika makala ya leo nakwenda kukushirikisha kitu muhimu sana ambacho Vishen ametushirikisha kwenye kitabu chake, kitu hicho ni maeneo 12 ya kuwa na mlinganyo kwenye maisha yako ili uwe na mafanikio kamili na yanayogusa kila eneo la maisha yako.

maeneo 12 ya mafanikio

Katika maeneo haya 12, kila eneo tutaangalia vitu vinne; ULIPO SASA, UNAKOTAKA KUFIKA, VIWANGO VYA KUJIWEKEA NA KITABU CHA KUSOMA.

Karibu tujifunze maeneo haya 12 kwa kina, ili uweze kuchukua hatua kuleta mlinganyo kamili kwenye maisha yako na kuwa na maisha bora na yenye mafanikio yaliyokamilika.

ENEO LA KWANZA; MAPENZI.

Hili ni eneo linalohusu mahusiano yako ya kimapenzi na mwenza wako. Ni eneo muhimu sana kwa sababu hili linagusa kila eneo la maisha yetu. Kama mahusiano yako ya kimapenzi yako vizuri basi maisha yako yanakuwa vizuri. Lakini kama eneo hili lina matatizo, hutaweza kutuliza akili yako kwenye jambo lolote.

ULIPO SASA; Tafakari pale ulipo sasa kwenye mahusiano yako ya kimapenzi, je umeoa au kuolewa au upo peke yako? Na je kwenye hali ya mahusiano uliyopo, unayafurahia? Unayaelezeaje mapenzi? Ni kitu gani unatoa na kipi unapokea kutoka kwenye mahusiano yako ya mapenzi? Je unaamini mapenzi yanaleta maumivu? Je upo tayari kumpenda kweli mwenzako na kumwonesha kwamba unampenda? Je unajiona ni mtu unayestahili kupendwa kweli? Jiulize na kujipa majibu ya maswali hayo na yatakupa picha ya pale ulipo sasa.

UNAKOTAKA KUFIKA; Katika kuboresha zaidi mahusiano yako ya kimapenzi, unapaswa kuwa na picha ya wapi unataka mahusiano hayo yafike. Katika kutengeneza picha ya unakotaka kufika, jiulize na kujipa majibu ya maswali haya; je mahusiano bora ya kimapenzi kwako unataka yaweje? Pata picha ya mahusiano yenye mafanikio, mnawasilianaje, kuchukulianaje, vitu gani mnafanya pamoja na jinsi mnavyoyafurahia maisha pamoja. Kuwa na picha hii kila wakati na ifanyie kazi, itakusukuma kuwa bora zaidi.

VIWANGO VYA KUJIWEKA; Katika eneo la mapenzi unapaswa kujiwekea viwango ambavyo utavizingatia ili kuimarisha eneo hili. Viwango vya kujiwekea ni muda wa kuwa pamoja wewe na mwenza wako, inaweza kuwa kwenye mtoko mnaofanya pamoja, kufanya mazoezi pamoja na hata kuwa na ratiba ya kuwa na faragha nyinyi wawili pekee kwa ajili ya yale muhimu kwenu. Zingatia sana hili la kupata muda wa kuwa na mwenzako na weka kiwango cha muda huo.

KITABU CHA KUSOMA; Kujiweka vizuri kwenye eneo la mahusiano ya mapenzi soma kitabu kinachoitwa MEN ARE FROM MARS, WOMEN ARE FROM VENUS Kilichoandikwa Na John Gray. Kitabu hiki kitakufundisha jinsi ya kuishi na mwenzako.

ENEO LA PILI; URAFIKI.

Mahusiano ya urafiki ni muhimu sana kwenye mafanikio yako. Hapa unapaswa kuwa na watu wa karibu kwako, ambao mnashirikiana kwa mambo muhimu. Unapaswa kuwa na angalau watu watano unaowaamini na wanaokuamini, ambao kwa pamoja mnaelekea kwenye mafanikio makubwa.

ULIPO SASA; katika kujipima pale ulipo sasa, jiulize unaelezeaje urafiki? Je unaamini urafiki unaweza kuwa wa kudumu? Je unaona urafiki una manufaa kwa kila mmoja au marafiki wananufaika zaidi na wewe kuliko unavyonufaika nao?

UNAKOTAKA KUFIKA; katika kupiga hatua zaidi kwenye mahusiano ya urafiki, pata picha ya mafanikio katika mahusiano yako ya urafiki. Pata picha ya aina ya marafiki unaotaka kuwa nao, vitu ambavyo mnashirikiana kwa pamoja na yale mambo mnayofanya kwa pamoja pale mnapokutana kama marafiki. Jione ukitoa mchango mkubwa kwa marafiki zako na wewe ukinufaika nao pia.

VIWANGO VYA KUJIWEKEA; jiwekee viwango vya kuboresha mahusiano yako na marafiki zako, kwa kuwa na utaratibu wa kuwasiliana na marafiki zako angalau mara moja kila wiki. Pia kuwa na utaratibu wa kukutana na marafiki kwa shughuli na matukio mbalimbali yanayowaleta pamoja na kuimarisha mahusiano yenu.

KITABU CHA KUSOMA; soma kitabu kinaitwa HOW TO WIN FRIENDS AND INFLUENCE PEOPLE Kilichoandikwa Na Dale Carnegie. Kitakusaidia sana katika kuboresha mahusiano yako ya urafiki.

ENEO LA TATU; SAFARI.

Safari mbalimbali za kujifunza na kubadili mazingira ni muhimu sana kwa mafanikio yako. Unapotoka pale ulipozoea na kwenda maeneo mengine, unajifunza zaidi na hata kupata mtazamo wa tofauti na ule uliozoea.

ULIPO SASA; unapofikiria kuhusu safari, ni picha gani unaipata kwenye akili yako. Je unaamini unahitaji kujipanga sana na kuwa na fedha nyingi ndiyo uweze kusafiri? Je unaona hakuna kipya cha kujifunza katika kusafiri bali kujichosha tu?

UNAKOTAKA KUFIKA; pata picha ya wale ambao unaona wana safari na burudani, kisha jione na wewe ukiwa na safari na burudani kwenye maisha yako. Ni maeneo gani ambayo ungependa kutembelea kwa ajili ya kujifunza na hata kupata burudani? Orodhesha maeneo yote ambayo unasukumwa sana kuyatembelea ili kujifunza zaidi na ifanye hii kuwa ndoto unayoifanyia kazi.

VIWANGO VYA KUJIWEKEA; jiwekee viwango vya safari utakazofanya kwa mwaka na hata mapumziko ambayo utayachukua kwenye kazi au biashara yako. Panga kusafiri na kujifunza zaidi kupitia tamaduni za wengine.

KITABU CHA KUSOMA; soma kitabu kinachoitwa LOSING MY VIRGINITY kilichoandikwa na Richard Branson. Kitabu hiki kitakupa hamasa ya kuishi maisha bora kwa kuwa na safari matukio ya burudani wakati unafanyia kazi ndoto zako.

ENEO LA NNE; MAZINGIRA.

Mazingira yako yana mchango mkubwa sana kwenye mafanikio yako. Kuanzia nyumbani kwako, gari lako, eneo lako la kazi au biashara na eneo lolote ambalo unakuwepo unaposafiri.

ULIPO SASA; ni katika mazingira gani unajisikia furaha? Je umeridhika na pale unapoishi sasa na jinsi unavyoishi? Je unaamini unastahili kuwa na mazingira bora na ya kifahari, kuanzia nyumbani mpaka kwenye kazi zako?

UNAKOTAKA KUFIKA; tengeneza picha ya mazingira bora kwako, kuanzia nyumbani, kazini na popote unapokuwa. Kama usingekuwa na kikwazo chochote, hasa kifedha, ungeishi nyumba ya aina gani, ungeendesha gari ya aina gani na eneo lako la kazi lingekuwaje? Beba picha hii kila siku ya maisha yako na ifanyie kazi kuifikia.

VIWANGO VYA KUJIWEKEA; yafanye mazingira yako kuwa safi na yanayokupa hamasa zaidi. Fanya chumba chako kuwa safi, nyumba safi, mazingira masafi na hata eneo lako la kazi liwe safi na vitu vipangiliwe kiasi cha kuwa rahisi kupata chochote unachotaka kutumia.

KITABU CHA KUSOMA; soma kitabu kinachoitwa THE MAGIC OF THINKING BIG kilichoandikwa na David Schwarrz. Kitabu hiki kitakusukuma kuboresha maisha yako na kuwa na ndoto kubwa kuhusu nyumbani kwako, ofisini kwako na mengine mengi.

ENEO LA TANO; AFYA.

Afya ni kiungo muhimu sana kwa mafanikio yako, bila ya afya imara, mafanikio yoyote unayokuwa umeyapata ni kazi bure kwa kuwa hutaweza kuyatumia au kuyafurahia.

ULIPO SASA; unaielezeaje afya bora? Unaelezeaje ulaji wa kiafya? Je kwa afya uliyonayo sasa unajiona uko sahihi au unapaswa kuboresha zaidi? Je unaamini unaweza kuwa na afya bora na kuishi miaka mingi kadiri utakavyo?

UNAKOTAKA KUFIKA; pata picha miaka mitano, kumi na hata 20 ijayo, unajiona wapi kiafya? Ni ulaji wa aina gani na mazoezi ya aina gani utakayokuwa unafanya sasa ili yakufikishe kwenye picha yako ya kiafya. Jikumbushe picha hii kila siku ili uchukue hatua za kukufikisha kwenye picha hiyo.

VIWANGO VYA KUJIWEKEA; jiwekee viwango vya kiafya kama vile uzito ambao hupaswi kuuvuka, aina ya vyakula utakavyokula na vipi hutakula au kupunguza. Pia chagua aina ya mazoezi utakayokuwa unafanya na ratiba yako katika kuyafanya.

KITABU CHA KUSOMA; kwa wanaume soma kitabu kinachoitwa THE BULLETPROOF DIET cha Dave Asprey ambapo hapa utajifunza sayansi ya ulaji ya afya. Kwa wanawake soma kitabu kinachoitwa THE VIRGIN DIET kilichoandikwa na JJ Virngin ambapo utajifunza kuhusu ulaji na mazoezi.

ENEO LA SITA; AKILI.

Kila wakati unapaswa kukua zaidi kiakili, unapaswa kujifunza na kuwa bora zaidi. Elimu haiishi pale unapohitimu, bali ndiyo inaanza. Lazima uwe tayari kujifunza kila siku ili kuwa na mafanikio makubwa.

ULIPO SASA; ni kwa kiwango gani unajifunza vitu vipya? Je unakua kwa kiasi gani kadiri muda unavyokwenda? Ni vitabu gani na vingapi unavyosoma kwa wiki, mwezi na hata mwaka?

UNAKOTAKA KUFIKA; unataka kupiga hatua kiasi gani kiakili, unataka kuwa na maarifa na hekima kwa viwango gani? Je ni vitabu gani unapaswa kusoma ili kupata maarifa na hekima unayotaka kuwa nayo? Chukua hatua kila siku ili kufikia lengo lako la maarifa na hekima.

VIWANGO VYA KUJIWEKEA; weka utaratibu wa kukua zaidi kiakili kwa kujisomea kila siku. Chagua vitabu utakavyosoma na kila siku weka idadi ya kurasa za kusoma. Kurasa kumi kwa siku ni kitu ambacho kila mtu anaweza kusoma, na kila mwezi ukasoma kitabu kimoja.

KITABU CHA KUSOMA; hapa unapaswa kuboresha kazi na uwezo wako wa kujifunza, ili uweze kujifunza zaidi. Ili kuwa bora kwenye kujifunza, unashauriwa kupata kozi ya Jim Kwik kuhusu kujifunza, kozi hii inapatikana kwa kubonyeza hapa; How To Be A Super Learner | Jim Kwik (www.mindvalley.com/superbrain/masterclass/invite)

ENEO LA SABA; UJUZI.

Mambo yanabadilika kwa kasi sana, ujuzi wowote ulionao sasa unapitwa na wakati. Hivyo lazima uwe tayari kukuza na kuboresha zaidi ujuzi wako kadiri unavyokwenda.

ULIPO SASA; ni maeneo gani ambayo uko vizuri zaidi kwenye kazi au biashara yako? Je kwa ujuzi ulionao sasa, umekuwa unapiga hatua zaidi au umekwama hapo kwa miaka mingi? Kama hupigi hatua ni nini kinakukwamisha?

UNAKOTAKA KUFIKA; je ni ujuzi gani unaohitaji kuwa nao ili uweze kufanikiwa kwenye kazi au biashara unayofanya kwa muda mrefu ujao. Kama ungekuwa ndiyo unaanza elimu yako, je ni ujuzi gani ambao ungejifunza. Pata majibu ya maswali hayo na anza sasa kujijengea ujuzi unaoupenda na utakaokuwezesha kuwa bora zaidi kwenye soko.

VIWANGO VYA KUJIWEKEA; chagua vitabu na mafunzo ambayo yatakuwezesha kupiga hatua zaidi kwenye ujuzi wako. Kadiri unavyokwenda hakikisha unakuwa bora, unakuwa na ufanisi zaidi na uzalishaji wako unaongezeka.

KITABU CHA KUSOMA; soma kitabu 4 HOUR WORK WEEK kilichoandikwa na Timothy Ferris na utajifunza njia ya haraka ya kupata na kukuza ujuzi wowote.

ENEO LA NANE; IMANI.

Mafanikio kamili yanahusisha eneo la imani na kiroho. Lazima uwe unakua kiimani na kiroho ili kuwa na maisha yenye mlinganyo. Unapaswa kuwa na mambo unayofanya ili kuboresha imani yako, kama kujifunza, maombi, tahajudi na hata kuwa na shukrani kwa mambo mbalimbali.

ULIPO SASA; ni imani gani uliyonayo kwenye maisha yako? Ni vitu gani unavyofanya kila siku ili kuimarisha imani yako na kuweza kukua zaidi kiimani? Je imani uliyonayo umechagua mwenyewe au umeipokea kutoka kwa wazazi na jamii?

UNAKOTAKA KUFIKA; ungependa kupiga hatua zipi kubwa kiimani na kiroho? Unajionaje unapokuwa umefanikiwa sana kiroho? Ni hatua zipi zitakufikisha kwenye mafanikio zaidi ya kiroho. Je ungependa kuwa unafanya miujiza kwenye maisha yako. Yote haya yanawezekana iwapo utaweka juhudi kubwa kwenye ukuaji wa kiroho, kwa kujifunza, kusali na kufanya tahajudi kwa kina.

VIWANGO VYA KUJIWEKEA; tenga muda kila siku wa kuchukua hatua za kukua kiimani. Unaweza kutenga dakika 15 kila siku za kusali au kufanya tahajudi, na dakika nyingine 15 za kusoma eneo la imani.

KITABU CHA KUSOMA; soma kitabu CONVERSATIONS WITH GOD kilichoandikwa na Neale Donald ambacho kitakuwezesha kukua zaidi kiroho. Pia kitabu AUTOBIOGRAPHY OF A YOGI cha Paramahansa Yogananda kitakupa uelewa mkubwa wa kiimani.

ENEO LA TISA; KAZI.

Kazi au biashara unayofanya ni eneo muhimu sana la maisha yako. Hili ni eneo ambalo unapaswa kuwa unakua kadiri muda unavyokwenda. Kwa sababu kubaki pale pale, ni kurudi nyuma. Katika kazi au biashara unayofanya, lazima uweze kupima ukuaji wako.

ULIPO SASA; unaielezeaje kazi? Je unafurahia kazi au biashara unayoifanya? Je unajiona kuwa kwenye nafasi ya kufanikiwa kupitia kazi au biashara unayofanya. Je unakua kwa kiasi gani ukijipima kikazi na kibiashara?

UNAKOTAKA KUFIKA; ni ubobezi gani unajiona kuwa nao kwenye kazi unayofanya? Ni mabadiliko gani ungependa kuleta kupitia kazi au biashara unayofanya. Kuwa na picha ya mchango wako mkubwa na mabadiliko unayotaka kuleta na ifanyie kazi kila siku.

VIWANGO VYA KUJIWEKEA; jiunge na kundi la kitaalamu kulingana na taaluma au ujuzi ulionao. Shiriki mikutano na mafunzo mbalimbali yanayoendana na taaluma na ujuzi ulionao. Pia jipime jinsi unavyokua kupitia kazi au biashara unayofanya.

KITABU CHA KUSOMA; kitabu ORIGINALS cha Adam Grant ni kitabu kitakachokuwezesha kuwa na ubunifu mkubwa kwenye kazi yako na kufikiria nje ya boksi, kuuza mawazo yako na kuleta mapinduzi.

ENEO LA KUMI; UBUNIFU.

Unapaswa kuwa na kitu cha kibunifu unachofanya kwenye maisha yako. Kitu hiki kinachochea akili yako kufikiri zaidi na kukuwezesha kukua zaidi. Inaweza kuwa uandishi, uchoraji, uimbaji, upigaji vifaa vya muziki, uigizaji na kadhalika.

ULIPO SASA; je unaamini kwamba wewe ni mbunifu? Je kuna mtu mbunifu ambaye unapenda sana kuwa kama yeye? Ni mambo gani ya kibunifu ambayo unafanya sasa kwenye maisha yako? Je ni vipaji gani ulivyonavyo na unavitumiaje?

UNAKOTAKA KUFIKA; ni ubunifu gani ambao ungependa kuwa nao na kubobea zaidi siku zijazo? Ni jinsi gani unaweza kutumia ubunifu huo kuwasaidia wengine zaidi. Chagua ubunifu unayotaka kuwa nao na jiendeleze kila siku na kutoa mchango kwa wengine.

VIWANGO VYA KUJIWEKEA; chagua aina ya ubunifu ambao utakuwa unajihusisha nao na kila siku tenga muda wa kujiendeleza kwenye ubunifu huo. Unaweza pia kujiunga na wengine au kushiriki madarasa yanayokuwezesha kukuza zaidi ubunifu wako.

KITABU CHA KUSOMA; soma kitabu THE WAR OF ART cha Steeven Pressfield ambacho kitaamsha na kuchochea ubunifu uliopo ndani yako na kuweza kufanya kazi za kibunifu.

ENEO LA KUMI NA MOJA; FAMILIA.

Familia yako ni mahusiano ambayo ni muhimu sana kwenye maisha yako. Haya ni mahusiano ambayo yana mchango mkubwa sana kwenye mlinganyo wako wa mafanikio. Kadiri mafanikio haya yanavyokuwa bora, ndivyo unavyokuwa bora.

ULIPO SASA; je unafurahia kurudi nyumbani baada ya siku yako ya kazi kuisha? Je unajua lipi jukumu lako kuu kwenye familia? Na je familia kwako ni watu gani? Unaamini familia ni mzigo kwako au kichocheo kwako kufanikiwa?

UNAKOTAKA KUFIKA; pata picha ya familia bora kwako, inawahusisha watu gani, mahusiano yapoje na kila mtu ana mchango gani kwenye familia hiyo? Weka juhudi katika kujenga familia hii bora kwako na siyo kuishi kwenye familia usiyoifurahia.

VIWANGO VYA KUJIWEKEA; weka lengo la kutenga muda wa kufanya mambo ya kifamilia. Tenga muda wa kuwa pamoja na familia, mfano mzuri ni kuwa na chakula cha pamoja, kutoka pamoja au kwenda kutembelea ndugu na jamaa kama familia. Haya yanaimarisha mahusiano ya kifamilia.

KITABU CHA KUSOMA; kitabu MASTERY OF LOVE cha Don Miguel Ruiz kitakupa msingi mkuu wa mafanikio kwenye familia ambao ni upendo.

ENEO LA KUMI NA MBILI; JAMII.

Unaishi kwenye jamii, na hivyo mafanikio yako hayajakamilika kama hayaigusi jamii inayokuzunguka. Unapaswa kuwa unatoa kwa jamii yako, ili inufaike na mafanikio yako pia. Hata kile unachofanya (kazi au biashara), lazima kiwe na manufaa kwa jamii.

ULIPO SASA; je unaamini kwenye maadili ya jamii uliyopo? Je unajua ni nini kusudi kubwa la jamii uliyopo? Je unaamini kwamba una mchango kwenye jamii yako? Na je una mchango kiasi gani kwenye jamii yako?

UNAKOTAKA KUFIKA; chagua jamii ambayo unataka kuwa na mchango, inaweza kuwa majirani zako, marafiki, mtaa, mji, nchi na hata dunia kwa ujumla. Unajiona ukiwa na mchango gani kwenye jamii yako. Angalia uwezo na vipaji ulivyonavyo na jiulize ni kwa namna gani jamii inanufaika navyo. Kila siku chukua hatua ya kuifanya jamii kuwa bora zaidi.

VIWANGO VYA KUJIWEKEA; chagua maeneo ambayo ungependa kutoa mchango wako kwa jamii kisha weka utaratibu wa kutoa mchango huo. Iwe ni kupitia misaada mbalimbali, kujitolea na hata kazi unayofanya kuwa na manufaa kwa jamii yako.

KITABU CHA KUSOMA; soma kitabu kinachoitwa DELIVERING HAPPINESS kilichoandikwa na Tony Hsieh, kitakufundisha jinsi ya kutoa mchango mkubwa kwa jamii na dunia kwa ujumla kupitia kazi au biashara unayofanya.

Rafiki, haya ndiyo maeneo 12 ya kuweka mlinganyo kwenye maisha yako ili uwe na mafanikio makubwa na maisha yenye furaha. Usipuuze hata eneo moja, kwa sababu kushindwa kwenye eneo moja, kutayavuruga sana maisha yako.

Katika makala ya tano za juma nitakushirikisha kanuni kumi za kuchagua kuishi ili uwe na maisha ya tofauti na uweze kuwa na mafanikio makubwa. Pia nitakushirikisha aina bora ya tahajudi unayoweza kuifanya kwa dakika 15 pekee kwa siku na ikakuwezesha kukua zaidi kiroho na hata kuvuta chochote unachotaka kwenye maisha yako.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge