Waswahili wanasema mambo mazuri hayahitaji haraka na pia wanaendelea kusisitiza haraka haraka haina baraka.
Ni kweli misemo hii miwili ina ukweli mkubwa ndani yake, kwamba ili upate mambo mazuri, lazima uwe na subira. Vitu vizuri kwenye maisha vinahitaji muda zaidi.
Kuna vitu hata kama una uwezo wa kuvifanya kwa haraka, havitakuwa na matokeo mazuri kama ungevifanya kwa utulivu na subira.
Lakini pia subira imekuwa kichaka cha wengi kujificha, pale ambapo watu wanakuwa na hofu ya kuanza kitu, pale ambapo wanajiona hawajawa tayari kuanza, basi hujificha kwenye kichaka cha kuwa na subira. Unajiambia kwamba unajipa subira kumbe ukweli ndani yako ni unajificha, una hofu ambayo huwezi kuivuka.
Swali ni je unawezaje kutofautisha subira ya kweli na kujificha?
Na jibu ni moja tu, hatua zipi ambazo tayari umeshachukua? Kama hakuna hatua yoyote ambayo umeichukua kwenye kile unachotaka, kama hakuna nguvu, muda wala fedha ambao umeshawekeza kwenye kitu, hapo huna subira, bali unajificha.
Hata kama unahitaji subira, lazima uwe umeshachukua hatua fulani, na lazima kuna hatua unakuwa unaendelea kuchukua, ambacho hutegemei ni matokeo makubwa ndani ya muda mfupi, lakini hatua unaendelea kuchukua.
Kila kitu kinahitaji sisi kuchukua hatua ili kiweze kuleta matokeo, iwe ni ya muda mfupi au muda mrefu. Hivyo usiwe mtu unayejificha na kujidanganya unahitaji muda, badala yake achana na muda, wewe weka kila aina ya juhudi unayopaswa kuwekwa, ila tu usilazimishe matokeo yaje kwa haraka uliyonayo wewe.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ahsante kocha hapa kunahtajika kukwepa mtego wa kusema una vuta subira kumbe n kujificha malengo yangu niyavunje vunje katika hatua ndogo ndogo
LikeLike
Hakika,
LikeLike