Rafiki yangu mpendwa,

Kwa zaidi ya miaka sita nimekuwa kwenye tasnia hii ya kuanzisha na kuendesha blogu mbalimbali. Na pia nimekuwa natumia blogu hizo kuingiza kipato.

Nimekuwa pia nawashirikisha watu jinsi ya kuanzisha blogu zao na jinsi ya kuzitumia kutengeneza kipato. Niliandika kitabu JINSI YA KUTENGENEZA KIPATO KWA KUTUMIA BLOG, ambacho kimewasaidia wengi kuanzisha blogu zao.

KIPATO KWA BLOG

Lakini naona changamoto kubwa kwa wengi, wengi wameanzisha blogu zenye mafanikio kwa kuwa na wasomaji, lakini haziwaingizii kipato. Kila wanapojaribu kuingiza kipato kupitia blogu hizo wanashindwa.

Katika kuchunguza ni wapi wengi wanakwama, nimegundua yapo maeneo manne yanayowakwamisha wengi. Kama kila mwandishi wa blogu atazingatia maeneo haya manne, basi atakuwa na blogu yenye mafanikio na inayokuingizia kipato.

MOJA; UJUMBE KAMILI NA UNAOELEWEKA.

Eneo kubwa ambalo wengi wanakwama ni kukosa ujumbe kamili na unaoeleweka. Watu wengi wanaanzisha blog bila ya kuwa na ujumbe mmoja ambao wanataka kufikisha kwa wasomaji wao. Hivyo kinachotokea ni blogu inakuwa na kila aina ya ujumbe, na wasomaji hawawezi kuitofautisha na blog nyingine.

Unapoanzisha blogu, anza na ujumbe kamili na unaoeleweka, ambao unamfanya msomaji awe ana kitu anachotegemea kuja kwako. Blog yako isiwe kama jalala ambalo linabeba kila kitu. Chagua kitu kimoja ambacho kitaibeba blog hiyo na kuitofautisha na blog nyingine.

Nilipoanzisha AMKA MTANZANIA kusudi lake lilikuwa kutoa maarifa ya mtu kujitambua na kuweza kushika hatamu ya maisha yake. Mtu aache kulalamika na badala yake achukue hatua ili kuyafanya maisha yake kuwa bora, kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wa kila mtu.

Chagua ni ujumbe upi mkuu ambao blog yako inabeba na simamia huo kwa kuutoa kwa namna ambayo msomaji atakuelewa.

MBILI; KUWA NA JUKAA MAALUMU NA NJIA BORA YA KUSAMBAZA UJUMBE WAKO.

Kumekuwa na kelele nyingi zama hizi, na mitandao ya kijamii imekuwa inazidisha kelele hizi. Watu wengi wamekuwa wanatumia muda mwingi kwenye mitandao hii na hilo linawasukuma waandishi wengi kuona njia sahihi ya kuwafikia wasomaji ni kwa mitandao ya kijamii. Kwa njia hii wanatumia muda mwingi kutafuta ‘likes’ na ‘followers’ kwenye mitandao ya kijamii kuliko muda wanaotumia kukuza ufuasi na usomaji kwenye blog zao.

Mitandao ya kijamii ni kama kijiweni tu ambapo watu wanakutana, lakini mwisho wa siku wanarudi majumbani kwao. Hivyo unapaswa kuweka nguvu zako nyingi katika kutengeneza nyumba yako ambayo ni blog kuliko unazoweka kwenye vijiwe ambavyo ni mitandao ya kijamii.

Kazana kujenga jukwaa ambalo watu wanalitembelea na kulitegemea katika kujifunza. Maarifa yote muhimu yaweke kwenye blog na siyo kutegemea mitandao ya kijamii pekee kwa sababu unapata ‘likes’ na ‘followers’ wengi. Inapokuja kwenye kutengeneza kipato mtandaoni, likes na follows hazina umuhimu kama wasomaji wanaokuamini na kukufuatilia.

Kupitia AMKA MTANZANIA nimekuwa naweka nguvu nyingi kuandaa makala bora za kwenda kwenye blog na kwenye email list pia. Email list ni mfumo wa kuwatumia watu mafunzo moja kwa moja kwenye email zao, kitu ambacho kinaongeza uaminifu na watu kuwa tayari kununua kile unachouza, kwa kuwa wameshajifunza zaidi kutoka kwako.

TATU; WATU WANAOKUAMINI NA KUKUFUATILIA.

Umuhimu wa kutengeneza jukwaa ni kuwapata watu wanaokuamini na kukufuatilia. Watu watakaokuuliza mbona siku hizi hatupati mafunzo pale utakapocha kuandika. Lakini acha kuweka vitu kwenye mitandao ya kijamii na hakuna atakayekuuliza.

Kazi yako kubwa ni kutengeneza wafuasi, wasomaji ambao wanaielewa kazi yako, wanaamini kwenye ujumbe wako na wapo tayari kwenda na wewe katika safari yako ya kuwa bora kwenye kile unachofanya.

Wasomaji wa aina hii ndiyo ambao watakuwa wateja wako, kwa kulipia bidhaa na huduma mbalimbali ambazo utakuwa unazitoa.

Muda wote nimekuwa naweka nguvu nyingi kutengeneza jamii ya tofauti ya watu ambao wanataka kupiga hatua zaidi kwenye maisha yao kupitia AMKA MTANZANIA. Mwaka 2018 nilijitoa kwenye mitandao yote ya kijamii, ambapo nilikuwa na wafuasi wanaozidi elfu 10, lakini mpaka sasa ni watu wasiozidi kumi ambao wamewahi kuniuliza mbona siku hizi hatukuoni kwenye mitandao. Lakini nisipoandika kwa siku chache tu, napokea jumbe nyingi za watu wakitaka kujua kwa nini hawapati mafunzo.

NNE; BIDHAA AU HUDUMA YA KUUZA ILI BLOG YAKO IWEZE KUJIENDESHA.

Hapa ndipo muhimu na ambapo wengi wanakwama. Mtu anaanzisha blog akiwa hana wazo kabisa atauza nini kupitia blog hiyo. Hivyo anakazana kupata wasomaji, anakuwa nao, ila hajui awauzie nini.

Unapaswa kuwa na wazo la bidhaa au huduma utakayouza kupitia blog yako, mapema kabisa unapoanza. Hata kama hutaanza kuuza mwanzoni, lakini lazima hilo liwe kwenye mawazo na mipango yako.

Kwa kuwa na wazo hili, kila unachofanya kitalenga kukusogeza karibu zaidi na mpango wako wa kuuza kupitia blog yako. Pia utaacha kuyumbishwa na watu ambao wanakuja kwako na mawazo mbalimbali ambayo siyo sahihi kwako. Kwa mfano kama lengo la blog yako ni kutoa mafunzo kisha wale unaowafundisha watake zaidi na hapo wanunue huduma zako nyingine, utaandaa mafunzo ya ziada kwa wale wanaotaka zaidi na hutapokea matangazo kwenye blog yako.

AMKA MTANZANIA ndiyo malango wa kwanza mimi kukutana na wewe, baada ya kujifunza bure kabisa na kuona maarifa hayo yanakufaa, nina huduma na bidhaa mbalimbali ambazo unaweza kulipia na ukanufaika zaidi;

  1. Kuna vitabu mbalimbali vya mafanikio, nimeshaandika vitabu nane, unaweza kupata orodha ya vitabu hivyo kwa kubonyeza hapa.
  2. Kuna huduma ya KISIMA CHA MAARIFA ambapo unapata nafasi ya kuwa kwenye kundi pekee la wasap ninaloendesha na kutoa mafunzo kila siku, unaweza kupata maelezo yake zaidi kwa kubonyeza hapa.
  3. Kuna huduma za ukocha binafsi ambazo natoa kwa wale waliokwama na wanataka kupiga hatua zaidi kwenye maisha yao. Maelezo yake zaidi yanapatikana kwa kubonyeza hapa.
  4. Kuna semina kubwa ya mwaka, ambayo huwa inafanyika mara moja na inakuwa nafasi pekee ya sisi kukutana ana kwa ana na kujifunza.
  5. Kuna huduma ya usomaji wa vitabu, ambapo unapata uchambuzi wa kina wa vitabu kila juma, maelezo zaidi bonyeza hapa hapa.

Hivyo hakikisha unapokuwa na blog, una kitu cha kuuza. Kwa sababu utakapokuwa unatengeneza wasomaji wako, wapo ambao watataka vitu zaidi kutoka kwako. Pia unapouza, chagua maeneo machache ya kubobea na siyo kukubali kila kitu ambacho watu wanataka uwauzie au uwafanyie.

Rafiki, nina imani makala ya leo imekuongezea kitu katika kukuwezesha kuanzisha na kukuza blog yako na kuitumia kutengeneza kipato.

Kama bado hujawa na blog, anza kwa kusoma kitabu JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, kitabu ni softcopy na kinatumwa kwa email, gharama yake ni tsh elfu 10 (10,000/=) kupata kitabu tuma fedha kwa namba 0717396253 au 0755953887 kisha tuma email yako na utatumiwa kitabu.

Pia huwa nawaandalia watu blog za kitaalamu, ambapo unapata blog ambayo tayari imetengenezwa na wewe ni kuitumia tu. Kwa maelezo zaidi kuhusu blog za mtaalamu bonyeza hapa.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge