Kuna njia mbili za kuyaendesha maisha yako,
Njia ya kwanza na inayopendwa na wengi ni njia ya kuonekana, hapa unafanya vitu ili uonekane na wengine kwamba unafanya. Hivyo unafanya kile ambacho wengine wanafanya, na unafanya zaidi vitu vinavyoleta matokeo ya muda mfupi hata kama vina madhara kwa muda mrefu. Njia hii imepata nguvu kubwa katika zama hizi za mitandao ya kijamii, ambapo kila mtu sasa ni chombo cha habari. Watu wanaweza hata kuonekana wameshika kitabu, siyo kwa sababu wanakisoma na kukua, bali kwa sababu wanataka waonekane wanasoma vitabu.
Njia ya pili ni kukua, hii ni njia ambayo inapendwa na wachache, kwa kuwa haina mbwembwe. Hapa unafanya kitu ili kukua, ili kupiga hatua zaidi, kutoka pale ulipo sasa na kwenda mbele zaidi. Kwa njia hii unafanya viti vya tofauti, ambavyo wengine hawafanyi na wala wengi hawaelewi. Unafanya vitu ambavyo vinaweza visiwe na manufaa leo, lakini siku zijazo vinakuwa na manufaa makubwa. Hii ni njia inayomjengea mtu uwezo mkubwa wa kufanikiwa zaidi baadaye.
Kaa chini na jifanyie tathmini, pitia kila ambacho unafanya kwenye maisha yako, na jiulize je unafanya kuonekana au unafanya kukua. Ukishapata picha kamili, achana na yale yote unayofanya ili kuonekana na hamishia nguvu zako kwenye yale unayofanya ili kukua.
Uzuri ni kwamba unapoweka nguvu zako kwenye ukuaji, utakua zaidi na watu sahihi watakuona. Lakini unapoweka nguvu zako kwenye kuoneka, watu wanajifunza kukupuuza.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,