Tumekuwa tunachagua kuyapoteza maisha yetu wenyewe kwa kuweka mkazo kwenye maeneo ambayo siyo sahihi.

Mara nyingi tumekuwa tunaangalia mwisho wa safari yetu, kisha kujiambia kama tukifika pale basi tutakuwa na furaha kubwa na maisha yetu yatakuwa mazuri sana.

Tunakazana kweli kweli, tunaweka maisha mengine pembeni na kuhakikisha tunafika pale tulipopanga kufika, na kweli kwa juhudi tunafika. Lakini hatupati furaha ambayo tulitegemea kupata, hatuoni cha tofauti sana baada ya kupata tulichopigania sana.

Na hapo tunaona labda tulichokuwa tunafanyia kazi siyo sahihi na hivyo tunachagua tena kitu kingine cha kufanyia kazi, kama bado tuna muda na nguvu. Lakini matokeo tunayopata ni yale yale, hakuna mabadiliko makubwa tunayoyaona kwa kufika mwisho wa safari, na hivyo tunaona kama safari nzima haikuwa na maana.

Rafiki, kila safari uliyonayo kwenye maisha yako ina maana kubwa sana, lakini unapoteza maana hiyo pale unapoangalia mwisho wa safari badala ya kuangalia safari yenyewe.

Maana ipo kwenye safari yenyewe, furaha ipo kwenye safari yenyewe na siyo mwisho wa safari. Yale unayofanya kwenye kila hatua unayopiga, ndiyo yanatengeneza maana na furaha kwenye maisha yako.

Hivyo rafiki, weka juhudi kwenye kila unachofanya na siyo mwisho wa safari, kila hatua unayochukua tambua ndiyo hatua muhimu kwako katika kujenga maana na furaha kwenye maisha yako.

Kazi unayoifanya, wakati wa kuifurahia ni sasa unapokuwa unaifanya na siyo kusubiri mpaka unapostaafu. Ukisubiri mpaka kustaafu utakuja kugundua ulichokuwa unasubiria hakina maana kubwa kama uliyopoteza wakati wa ufanyaji wa kazi hiyo.

Biashara unayofanya sasa ndiyo maana na furaha yako iko ndani yake, kwa zile hatua unazopiga kila siku. Usisubiri mpaka ufikie mafanikio makubwa uliyopanga kufikia ndiyo ufurahie au kuona maana ya biashara hiyo.

Kila unachofanya kwenye kila siku ya maisha yako ndiyo kimebeba maana kwako, ndiyo kina furaha kwako. Kama hutaweza kupata maana kwenye kile unachofanya kila siku, kama huwezi kukifurahia basi jua hata kile unachotegemea kupata mwishoni hakitakupa maana wala furaha unayotegemea.

Ili kila siku yako kwa ukamilifu yako, kwa kupata maana na furaha kwa kila unachofanya na siyo kusubiri mpaka matokeo ya mwisho. Maisha yenye maana na furaha ni yale ambayo yana siku nyingi zenye maana na furaha kwako. Tengeneza siku hizo kila siku na utakuwa na maisha bora sana.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha