Habari za leo rafiki yangu mpendwa?

Karibu kwenye makala yetu ya leo ambapo tunakwenda kujifunza ukweli kuhusu sukari na madhara yake kwenye mwili. Kama kicha kinavyoeleza, sukari ni madawa ya kulevya yaliyohalalishwa, ni kitu chenye madhara makubwa sana kwenye afya zetu, lakini tumekuwa hatuelezwi wazi. Karibu kwenye makala hii ambayo itakupa mwanga mkubwa kuhusu sukari na hatua sahihi kwako kuchukua ili kuwa na afya bora.

sugar adiction

MAKUNDI YA VYAKULA.

Vyakula vyote tunavyokula, vimegawanyika katika makundi makubwa manne kutokana na virutubisho ambavyo tunapata kutoka kwenye vyakula hivyo.

Kundi la kwanza ni wanga na sukari, kundi hili huupa mwili virutubisho vinavyotumika kwenye kuupa mwili nguvu na kujenga mwili pia.

Kundi la pili ni mafuta, hili ni kundi linalotoa virutubisho muhimu kwa kuupa mwili nguvu na haya kutengeneza kemikali muhimu mwilini kama homoni.

Kundi la tatu ni protini, kundi hili huupa mwili virutubisho vinavyohitajika katika kuujenga mwili na kuponesha majeraha mbalimbali.

Kundi la nne ni mbogamboga, hili ni kundi ambalo linaupa mwili nyuzinyuzi zinazosaidia mfumo wa umeng’enyaji wa chakula pamoja na kuupa mwili vitamini na madini mbalimbali.

Katika makundi haya manne, wanga na sukari ndiyo kundi ambalo limekuwa linatumika na kupendwa sana na sisi binadamu, na hapa ndipo matatizo mengi kiafya yanapoanzia.

KWA NINI SUKARI INAPENDWA SANA NA BINADAMU.

Katika historia ya mageuzi na maendeleo ya binadamu, tumepitia zama mbalimbali. Na katika kipindi kikubwa katika zama hizi, maisha yalikuwa na hatari kubwa. Binadamu waliishi porini na hivyo hatari za wanyama na mazingira zilikuwa kubwa sana.

Hivyo kila wakati mtu alipaswa kuwa kwenye hali ya kupambana au kukimbia. Mtu akiwa porini na kusikia kishindo, hakusubiri mara mbili ili ajue kishindo ni cha nini. Badala yake mwili ulizalisha kemikali ya msongo, ambayo ilifanya mwili upate nguvu ya kutosha na kuanza kukimbia au kupambana na chochote kinachosababisha kishindo hicho.

Sasa kwenye makundi manne ya chakula tuliyojifunza hapo juu, wanga ndiyo kundi ambalo ni rahisi kuvunjwa na mwili na kutumika kuzalisha nguvu ya kupambana au kukimbia. Hivyo ili kuweza kupona, binadamu tulijifunza kutegemea zaidi wanga na sukari katika kupata nguvu za kukimbia au kupambana na hatari za mazingira.

Na kwa kuwa mazingira hayakuwa bora na upatikanaji wa wanga na sukari ulikuwa adimu, basi ubongo wa binadamu uliweka kipaumbele cha kwanza katika kupata sukari na ilipopatikana basi ubongo ulifurahia sana hilo.

KWA NINI SUKARI NI MADAWA YA KULEVYA YALIYOHALALISHWA.

Pamoja na madhara makubwa ya kiafya ya utumiaji wa sukari tutakayojifunza hapo chini, sukari haina tofauti kubwa sana na madawa ya kulevya kama kokeini au heroine.

Hii ni kwa sababu matumizi ya sukari yamedhibitishwa kusisimua sehemu za ubongo ambazo zinasisimuliwa na madawa hayo. Pale mtu anapotumia sukari, ubongo unasisimka na kuzalisha homoni inayoitwa dopamine, hii ni homoni ambayo huwa inaleta raha na kumsukuma mtu kurudia tena kile alichofanya.

Hivyo unapotumia sukari, ubongo unazalisha dopamine, ambayo inakufanya ujisikie vizuri na upate utamu wa sukari. Lakini baada ya hapo unasukumwa kutumia tena sukari ili upate utamu zaidi na kujisikia vizuri zaidi.

Hii ndiyo sababu watu wamekuwa wanapata msukumo mkubwa sana wa kutumia kitu chenye sukari, na wakishatumia mara moja hawawezi kuacha, wanatumia tena na tena na tena.

Matumizi haya ya sukari yanaleta hali ya uteja au uraibu ambao ni mgumu sana kuuvunja. Kila mtu anapoona kitu cha sukari akili yake haifikirii kitu kingine chochote bali jinsi ya kupata sukari hiyo. Na anapoonja mara moja, hawezi kujizuia bali atataka tena na tena.

Tafiti zinaonesha pia ya kwamba matumizi ya sukari yamekuwa yanabadili tabia za watu. Muda mfupi baada ya kutumia sukari watu wengi huwa wakorofi, wenye hasira na wasio na subira. Sukari inawapa nguvu za ziada ambazo zinawasukuma kuzitumia kwa njia ambazo siyo sahihi. Mtu anapokuwa na sukari nyingi kwenye mwili huwa kwenye hali ya msongo kama mtu ambaye ametumia kilevi.

Hivyo kwa uwezo wa sukari kusisimua ubongo kama madawa mengine, kitendo cha watu kuwa tegemezi kwenye sukari na kuadilika kwa tabia baada ya mtu kutumia sukari, kunaifanya sukari kuwa kwenye kundi moja na madawa ya kulevya.

KWA NINI MATUMIZI YA SUKARI YAMEPATA UMAARUFU MKUBWA?

Kwenye miaka ya 1950s mwanasayansi Ancel Keys alitikisa ulimwengu wa ulaji kwa kuonesha matokeo ya tafiti yanayosema ulaji wa mafuta ndiyo unaosababisha magonjwa ya moyo. Habari hiyo ilipokelewa kwa shauku na wafanyabiashara wa vyakula walitumia utafiti huo kuondoa kabisa vyakula kwenye mafuta na kuweka sukari zaidi. Na tangu hapo watu wamekuwa wanakula vyakula zaidi, lakini matatizo ya moyo ndiyo kwanza yamepamba moto.

Baadaye ilikuja kujulikana kwamba utafiti wa Ancel haukuwa sahihi, lakini jamii ikishaamini kitu ni vigumu sana kuwaaminisha tofauti. Hivyo mpaka leo watu wanaamini ulaji wa mafuta kidogo ni mzuri kiafya.

Tafiti mpya zinaonesha kwamba ulaji wa sukari una hatari kubwa kuliko ulaji wa mafuta au makundi mengine ya chakula. Unene uliopitiliza, kuziba kwa mishipa ya damu ni madhara yanayotokana na matumizi makubwa ya vyakula vya wanga na sukari.

SOMA; Imani Kumi (10) Potofu Kuhusu Ulaji Zinazowazuia Watu Kupunguza Uzito Na Kuwa Na Afya Bora.

KWA NINI SUKARI NI SUMU MBAYA SANA KWA MWILI WAKO.

Kama kuna kitu kimoja ambacho kila mtu anapaswa kuambiwa na kukielewa ni kwamba matatizo yetu mengi ya kiafya yanatokana na ulaji wa sukari. Kwa kifupi sukari ni sumu kubwa sana kwenye miili yetu. Japo tunaiona tamu na tunaipenda sana, lakini hakuna kinachotuua kama sukari.

Sukari ya kawaida tunayotumia inaitwa sucrose, ndani yake ina sukari rahisi za aina mbili, glucose na fructose. Glucose ndiyo sukari inayotumika kwa urahisi na mwili na hata ubongo katika kuzalisha nguvu. Fructose huwa haitumiki sana kuzalisha nishati, badala yake inageuzwa kuwa mafuta na kuhifadhiwa kwenye mwili. Na aina hii ya sukari rahisi ndiyo inachangia sana kwenye magonjwa ya moyo na mishipa ya damu kama kukomaa na kujaa mafuta kwenye mishipa hiyo kitu kinacholeta shinikizo la juu la damu (presha).

Ubaya zaidi wa sukari uko hapa, unapokula chakula cha sukari au wanga, sukari ni rahisi kumeng’enywa, hivyo muda mfupi baada ya kutumia sukari, kiwango cha sukari kwenye damu yako kinakuwa juu sana. Hali hii inachochea mwili kuzalisha homoni inayoitwa Insulin, ambayo kazi yake ni kuondoa sukari kwenye damu na kuihifadhi kwenye seli za mwili na nyingine kugeuzwa kuwa mafuta kwenye ini. Sasa kwa kuwa sukari imepanda kwa wingi kwenye damu, insulini inayozalishwa inakuwa nyingi pia, kitu ambacho kinapelekea sukari kwenye damu kushuka haraka. Hii inaleta hali ya mtu kujisikia uchovu na kutamani kula kitu cha sukari muda mfupi baada ya kula sukari.

Kama umekuwa unakunywa chai yenye sukari asubuhi, utakuwa unaliona hili mara kwa mara, saa moja baada ya kutumia sukari unajisikia kuchoka choka na unatamani kitu chochote chenye sukari. Hapa ndipo wengi wanakunywa soda au hata kula pipi, ili mradi tu kutuliza lile hitaji la mwili la kutaka sukari ya haraka.

HATUA SAHIHI KWAKO KUCHUKUA KUHUSU SUKARI.

Rafiki, kama kuna hatua moja ambayo unapasa kuichukua, hata kama utashindwa kuchukua hatua nyingine zozote kwenye ulaji wako, basi ni kuachana kabisa na sukari. Yaani acha kabisa kutumia sukari, na utaupumzisha mwili wako na hali hii ya kutengeneza sumu ambazo zinakuchosha, kukuletea magonjwa na hata kukuzeesha haraka.

Vyakula vya sukari vya kuepuka ni kama ifuatavyo, sukari yoyote unayoongeza kwenye chai au chakula, asali, miwa na juisi yake, matunda yoyote yenye utamu wa sukari, soda, juisi za matunda hata kama ni asili, bia, mvinyo, bidhaa zozote za kiwandani ambazo zimetengenezwa kwa kuongezwa sukari, kama mikate, maandazi na chochote ambacho kimeongezwa sukari.

Pia punguza sana matumizi yako ya vyakula vya wanga, kwa kula kiasi kidogo sana na mara moja kwa siku, hasa mlo wa jioni au usiku. Sehemu kubwa ya chakula chako inapaswa kuwa mafuta sahihi, protini na mbogamboga.

Nyongeza; usidanganyike na vitu vitamu ambavyo unaambiwa havina sukari, mfano soda za dayati, hizi zina kemikali ambazo ni sumu kwenye mwili wako kama ilivyo sukari. Tofauti yake na soda nyingine ni kwamba hazipandishi sukari kwenye damu, lakini bado ni sumu.

Najua hili litakuwa limekustua sana, kwa sababu vyakula vingi hapo ndiyo unatumia kila siku. Lakini kutumia kila siku au kuzoea haifanyi kuwa sahihi. Tafiti za kisayansi na za lishe zinaonesha wazi kwamba mazoea yetu kwenye ulaji ndiyo kikwazo kwetu kuwa na afya bora. Hivyo tunapaswa kujifunza na kuchukua hatua sahihi ili tuwe na afya bora na maisha bora pia.

Kujitengenezea mfumo bora wa ulaji ambao utaondoa kabisa sukari na kupunguza wanga soma makala hii; Tano Za Juma Kutoka Kitabu BULLETPROOF DIET (Mfumo Bora Wa Ulaji Utakaokuwezesha Kupunguza Uzito, Kuwa Na Nguvu Na Umakini Mkubwa Na Kuwa Na Afya Bora)

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge