Hizi ni sumu nne kubwa za mafanikio makubwa. Ni mambo ambayo wengi wamekuwa wanafanya kwa mazoea, lakini ni kikwazo kikubwa sana kwa mafanikio yao.
Hupaswi kuwa na wasiwasi au mashaka juu yako. Unapojiwekea malengo na mipango yako, unapaswa kujiamini kwamba utayafikia. Usianze kujiwekea wasiwasi na mashaka, kwa sababu ukisharuhusu hali hizo, utakosa kujiamini na ukishakosa kujiamini hakuna hatua kubwa utakazoweza kupiga. Na pia utakapokutana na changamoto ambazo ni sehemu ya safari ya mafanikio, kama hujiamini, kama una wasiwasi na mashaka, huo ndiyo unakuwa mwisho wako.
Usijitelekeze wewe mwenyewe, hili linapelekea wengi kujisahau na kujipoteza kabisa. Jukumu la kwanza kwenye mafanikio yako ni kujiendeleza wewe binafsi, kujitambua na kujifunza zaidi ili kuwa na hamasa ya kuchukua hatua kubwa unazopaswa kuchukua ili kufanikiwa. Kujitelekeza wewe mwenyewe kutakuondoa kabisa kwenye safari ya mafanikio, kwa sababu mafanikio siyo kitu unachotafuta, bali kitu unachokivutia kwa aina ya mtu unayekuwa.
Usijidharau, usijione kwamba huna uwezo wa kufanya makubwa au kufika pale unapotaka kufika. Huwezi kufanikiwa kama unajidharau, kama unajiona huwezi kufika unakotaka au kupata unachotaka. Haijalishi mambo ni magumu kiasi gani, wewe una uwezo mkubwa sana ndani yako. Kamwe usijidharau, badala yake jiamini na kuwa mtu unayeweza kuwa. Pia usiogope wengine watakuchukuliaje pale unapochagua kuwa mtu unayetaka kuwa.
Usiwe na kiburi, kiburi kinakuzuia usijifunze zaidi. Usifike hatua ya kuona kwamba tayari unajua kila kitu na huwezi kujifunza kwa wengine, usijione tayari una kila kitu na hivyo huwezi kumtegemea mwingine. Kuwa mnyenyekevu mara zote, kuwa tayari kujifunza na kuwa tayari kusaidiwa na wengine, hili litakuwezesha kufanikiwa zaidi.
Epuka sumu hizo nne na utaweza kuwa na mafanikio makubwa sana kwenye maisha yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,