“Pay attention to what’s in front of you—the principle, the task, or what’s being portrayed.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 8.22

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari JINSI UNAVYOFANYA KITU KIMOJA NDIVYO UNAVYOFANYA KILA KITU…
Huwa tunafikiri tunaweza kuwa mtu wa aina fulani kwenye kazi na mtu wa aina nyingine kwenye maisha,
Huwa tunadhani tunavyofanya kazi au biashara zetu hakuathiri maisha yetu.
Lakini ukweli ni kwamba, chochote unachofanya kina athari kwenye maisha yako.
Jinsi unavyofanya kitu kimoja ndivyo unavyofanya kila kitu.

Kama huna uaminifu kwenye kazi au biashara yako, basi jua hutakuwa na uaminifu kwenye maisha yako.
Kama hujitumi kwenye kazi au biashara yako, basi jua hutajituma kwenye maisha yako.
Huwezi kujitofautisha kwenye kile unachofanya.
Jinsi unavyoiishi siku moja ndivyo unavyoziishi siku zote.

Jijengee viwango vya maisha yako, kisha ishi viwango hivyo kila siku na kwenye kila jambo unalofanya, liwe kubwa au dogo, muhimu au siyo muhimu.
Unapochagua kufanya chochote, basi kifanye kwa viwango vyako.

Kama umeajiriwa kwenye kazi ambayo huipendi na unajiambia unaifanya basi tu, lengo lako ni kwenda kujiajiri, nakuhakikishia hutaweza kutoka kwenye ajira hiyo, na hata ukitoka basi utakwenda kushindwa vibaya unapojiajiri.
Kwa sababu kile unachofanya kwenye kazi yako sasa, ndiyo utakachofanya kwenye biashara yako pia.
Kama unataka kweli kuondoka kwenye kazi uliyonayo sasa, kitu cha kwanza kufanya ni kuipenda kazi yako na kuweka juhudi kubwa mno. Kwa kufanya hivyo utajijenga kuwa imara, utakua zaidi ya kazi yako na ukienda kuanzisha chochote kitakuwa imara kwa sababu wewe ni mtu imara.

Jinsi unavyifanya kitu kimoja ndivyo unavyofanya kila kitu, jiwekee viwango vyako vya ufanyaji na viishi wakati wote.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujiwekea viwango bora vya ufanyaji na kuviishi.
#KuwaNaMsimamo, #IshiKwaViwango, #KuwaBoraKilaSiku

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha