“We like to say that we don’t get to choose our parents, that they were given by chance—yet we can truly choose whose children we’d like to be.”
—SENECA, ON THE BREVITY OF LIFE, 15.3a
Ni siku mpya,
Siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Tumeipata nafasi nyingine bora sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari CHAGUA UWE MTOTO WA NANI…
Watu wanapenda kulalamika kwamba hawakuchagua wazaliwe na wazazi wa aina gani.
Na wengi hupenda kusingizia kushindwa kwao kwenye maisha ni wazazi wao kushindwa kuwapa misingi sahihi ya maisha.
Ni kweli huwezi kichagua uzaliwe na wazazi gani,
Lakini unaweza kuchagua uwe mtoto wa nani.
Na kama umeshapata akili ya kuwalaumu wazazi wako kama chanzo cha wewe kuwa na maisha magumu, basi wajibu wa kuwa na maisha bora upo kwenye mikono yako, wazazi wako au asili yako haihusiki tena.
Tuna bahati kubwa sana kwamba watu waliotutangulia, walioweza kufanya makubwa sana kwenye hii dunia, walioweza kuanzia chini na kwenda mpaka juu, waliweza pia kukaa chini na kuandika jinsi walivyoweza kufanya hivyo.
Na kama hawakuandika wenyewe, basi wapo watu ambao waliandika kwa niaba yao.
Hivyo hapo ulipo, una uwanja mpana sana wa kichagua uwe mtoto wa nani, wa kuchagua nani awe menta wako na kujifunza kupitia maisha yake na yale aliyofanya.
Usilalamike tena kwamba ulikosa mwongozo mzuri, usilalamike kwamba huna mtu wa kukushauri vizuri.
Una utajiri wa maarifa ambayo yamehifadhiwa kwenye maandishi.
Kazi yako ni kuchagua nani awe menta wako kisha jifunze kila kitu kuhusu mtu huyo.
Angalia wapi unataka kwenda na maisha yako, angalia wapi unataka kufika, kisha chagua watu walioweza kufika pale na chagua kuwa mtoto wa watu hao, ukijifunza kila kitu kutoka kwao, mazuri ya kufanyia kazi na mabaya ya kuepuka.
Usisahau pia na wewe kuwa mfano mzuri kwa wengine, kwa kuwafanya wengine wawe tayari kujifunza kupitia wewe.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuchagua unataka kuwa mtoto wa nani na kisha kujifunza kupitia hao uliowachagua.
#UgumuWaMaishaNiUgumuWako, #ChaguaUweMtotoWaNani #UsilaumuYeyote
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1