Katika kusimamia ukweli, kuna vitu viwili ambavyo unapaswa kuvizingatia.
Kitu cha kwanza ni ukweli unaopaswa kusemwa au kusimamiwa. Hapa lazima mtu aujue ukweli kwa hakika, na siyo kwa kukisia au kwa hisia.
Kitu cha pili ni yule ambaye anapaswa kuambiwa ukweli, lazima awe tayari kupokea ukweli huo na kuufanyia kazi.
Sasa wote tunajua kwamba ukweli huwa unauma, hivyo huwa tunatumia kila njia kuukwepa ukweli, lakini hili halifanyi kweli huo kubadilika.
Siyo watu wote wapo tayari kupokea ukweli, hivyo unapaswa kuwa makini sana kabla hujatoa ukweli wako.
Mpumbavu hapendi kukosolewa na kuambiwa ukweli, anapenda kusifiwa na anapooneshwa ukweli anaupinga. Yupo tayari kujitetea na hata kukushambulia kwa kumwonesha ukweli.
Mwerevu hupenda ukweli, japo unaumiza, lakini anajua unamfanya kuwa bora zaidi. Hivyo huupokea na kuufanyia kazi.
Hii yote ni kukuambia kwamba, kuwa makini sana na wale unaowaambia ukweli, kwanza jua kama mtu huyo ni mpumbavu au mwerevu.
Kama ni mpumbavu kaa mbali naye na usijaribu kumpa ukweli, utaumia wewe zaidi ya unavyotegemea kumrekebisha yeye.
Hasa pale mpumbavu huyo anapokuwa ni mtu mwenye mamlaka au cheo juu yako, atakitumia vibaya na hilo litakuumiza.
Na kwa upende wa pili, usiwe mpumbavu, kuwa mwerevu, kuwa tayari kujifunza, kuwa tayari kuupokea ukweli.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,