“You must build up your life action by action, and be content if each one achieves its goal as far as possible—and no one can keep you from this. But there will be some external obstacle! Perhaps, but no obstacle to acting with justice, self-control, and wisdom. But what if some other area of my action is thwarted? Well, gladly accept the obstacle for what it is and shift your attention to what is given, and another action will immediately take its place, one that better fits the life you are building.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 8.32
Chukua nafasi hii kutoa shukrani zako za kipekee kwa siku hii nyingine mpya ambayo tumeiona.
Siyo kwa akili wala nguvu zetu, na wala siyo kwa ujanja wetu, bali ni kwa bahati tu tumeiona siku hii nyingine nzuri.
Njia bora ya kuitumia bahati hii tuliyoipata ni kwenda kuiishi siku hii ya leo kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA ambavyo vinatuwezesha kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari NI MCHAKATO…
Kuyajenga maisha yako ni mchakato wa muda mrefu, unafanya hatua kwa hatua.
Watu wengi hawajui na kukubaliana ma mchakato huu, badala yake wanataka siku moja waamke wakiwa wamefanikiwa.
Hapa ndipo zile ndoto za alinacha, za kulala masikini na kuamka tajiri zinapozaliwa.
Watu wengi wapo kwenye kazi au biashara zao kwa muda mrefu wakijiambia siku moja mambo yatakuwa mazuri tu.
Lakini miaka inaenda na siku moja hiyo haifikiwi.
Rafiki, hakuna siku moja ambayo manbo yatakuwa mazuri yenyewe kwa ghafla tu.
Bali mambo yanatengenezwa kuwa mazuri kwa mchakato, mchakato ambao unaufanyia kazi kila siku.
Kila siku unayoiishi ni nafasi ya wewe kupiga hatua ndogo kuelekea kwenye mafanikio yako, au kupiga hatua za kukupoteza zaidi.
Unafanikiwa kwenye maisha pale hatua ndogo unazopiga kila siku zinakuwa za kukupeleka kwenye mafanikio yako.
Na unashindwa pale hatua ndogo unazopiga kila siku zinakupoteza zaidi.
Chukulia mifano mingi kwenye maisha, utaona jengo kubwa kabisa limejengwa, lakini halijaota kama uyoga, ni tofali moja limewekwa baada ya tofali jingine na mwisho pakawa na jengo.
Chukulia pia matembezi marefu, hujikuti tu upo mwisho wa matembezi, bali hatua moja baada ya nyingine ndiyo zinakufikisha unakokwenda.
Hivyo pia ndivyo utakavyofanikiwa kwenye maisha yako, kwa kupiga hatua moja baada ya nyingine, kila siku kukazana kuwa bora zaidi, kila siku kupiga hatua bora zaidi ya ulizopiga siku iliyopita.
Kwa njia hii utakuwa na uhakika wa kufanikiwa, na siyo kwamba hutakutana na vikwazo na changamoto, utakutana navyo sana, lakini kwa kuwa na misingi sahihi, utavuka kila aina ya vikwazo na changamoto.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kupiga hatua za kukupeleka kwenye mafanikio yako makubwa.
#MafanikioNiMchakato #HakunaKinachotokeaKamaAjali #KuwaBoraZaidiKilaSiku
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1