Upo usemi kwamba adui mpende, ni usemi wa kifalsafa ambao unatuonesha umuhimu wa upendo kwa wale ambao wana uadui na sisi.
Leo nakwenda kukupa usemi mwingine muhimu sana ambao utakusaidia sana kwenye safari yako ya mafanikio.
Usemi huo ni anayekupinga mpende.
Ni usemi mzuri na muhimu kwenye safari yako ya mafanikio kwa sababu wale wanaokupinga hata kama wana nia mbaya na wewe, lakini kuna mambo watayaibua kuhusu wewe, ambayo yatakusukuma kuwa bora zaidi.
Iko hivi rafiki, kila mmoja wetu ana madhaifu yake, na ni vigumu sana mtu kuona madhaifu yako wewe mwenyewe.
Lakini pia wale wanaokupenda, wale wanaokubaliana na wewe, huwa hawapendi kukuumiza, na hivyo hawakuelezi ukweli kuhusu madhaifu yako.
Ila wale wanaokupinga hawakuonei huruma, wanayaeleza wazi madhaifu yako na hivyo wanakupa nafasi ya kujua wapi unakosea au kuyumba na hivyo kuweza kuwa bora zaidi.
Najua kama binadamu hatupendi kuoneshwa na kuambiwa tunakosea, na hata watu wakituonesha tunakosea, hatutaki tuonekane tumebadilika kwa sababu ya ukosoaji wao. Lakini hayo yote hayana msaada.
Ili kufanikiwa zaidi lazima uwe bora, lazima uyavuke madhaifu yako.
Wale wanaokupinga wanakupa msaada mkubwa sana wewe kuyajua madhaifu yako na kuweza kuyafanyia kazi. Hivyo wapende na waache waendelee kufanya kazi yao ya kukufanya wewe kuwa bora zaidi, japo hawajui hilo.
Usikasirike pale wengine wanapokupinga, badala yake angalia upingaji wao, je kuna eneo ambalo wamegusa na kweli una udhaifu? Kama ndiyo basi chukua hatua ya kuwa bora zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Hakika ni kweli kocha, naendelea kuamini kuwa hata adui zetu wanamchango mkubwa kwenye mafanikio ya maisha yetu, na hata manen uliyoyaeleza hapo juu ni funzo sana kwangu nikiwa na mifano sahihi.
LikeLike
Vizuri Beatus
LikeLike