“Every event has two handles—one by which it can be carried, and one by which it can’t. If your brother does you wrong, don’t grab it by his wronging, because this is the handle incapable of lifting it. Instead, use the other—that he is your brother, that you were raised together, and then you will have hold of the handle that carries.”
—EPICTETUS, ENCHIRIDION, 43

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari JARIBU MKONO WA PILI…
Kila kitu kinachotokea kwenye maisha yako kina mikono miwili,
Mkono mmoja unaweza kubeba nao kitu hicho,
Na mkono mwingine huwezi kubeba nao kitu hicho.
Lengo lako kwenye maisha ni kutumia mkono ambao unaweza kubeba nao kitu na siyo kuhangaika na mkono usioweza kubeba nao kitu hicho.

Kama ndugu yako amekukosea, kuna mikono miwili hapo, mkono wa kwanza ni ndugu yako na mkono wa pili ni amekukosea.
Ili kuboresha mahusiano yenu huwezi kubeba hilo kwa mkono wa amekukosea, kwa sababu utazidi kuona kwamba alichofanya ni kibaya sana kwako.
Unaoaswa kubeba hilo kwa mkono wa ni ndugu yako, ambaye mmezaliwa na kukua pamoja, hili linaonesha zaidi kinachowaleta pamoja na siyo kinachowatenganisha na hivyo mahusiano yenu nayakuwa bora zaidi.

Kama umefanya kitu na ukashindwa kupata matokeo ambayo ulitegemea kupata, usitumie mkono wa kushindwa, maana mkono huo utakukatisha tamaa na kukufanya uone huwezi kupiga hatua.
Badala yake tumia mkono wa kujifunza, kwamba umejifunza njia ipi siyo sahihi kwako kupata unachotaka, hivyo unapojaribu tena usitumie njia hiyo ambayo haikuleta matokeo uliyotegemea.

Maisha ni rahisi sana pale unapojua una uhuru wa kuchagua, na inapokuja kwenye yale tunayokutana nayo kwenye maisha, tutumie mkono sahihi kuyabeba, mkono ambao utatuwezesha kuwa bora na kupiga hatua zaidi.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kubeba kitu kwa mkono sahihi.
#JaribuMkonoMwingine #KwenyeKilaUgumuKunaNjia #TatuaTatizoAuAchanaNalo

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1