“Fortune doesn’t have the long reach we suppose, she can only lay siege to those who hold her tight. So, let’s step back from her as much as possible.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 82.5b–6

Ni siku nyingine mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari USISHINDANE NA ASILI…
Asili haina huruma,
Asili haijali unataka nini au umeonewa kiasi gani.
Asili inakwenda kwa kanuni na taratibu zake yenyewe, haijali kuhusu uwepo wako.

Hivyo usishindane na asili,
Kwa kwenda kinyume na kanuni za asili, ni wewe utakayeishia kuumia.
Inaweza isiwe sasa, lakini jua kuna wakati utalipa kila ambacho umefanya kinyume na kanuni za asili.

Kula sana leo kutimiza tamaa yako na hakuna tatizo utakaloliona haraka.
Lakini siku nyingi zijazo utakuwa na uzito uliopitiliza, utakuwa na magonjwa kama ya presha na kisukari na hapo ndipo utajua kwamba asili huwa haishindwi.
Tumia zaidi ya kipato chako leo, na ukitaka zaidi kopa na hakuna baya litakalotokea leo wala kesho.
Lakini baada ya muda utajikuta kwenye shimo kubwa la madeni na maisha kuwa magumu mno, huku ukikosa kabisa uhuru wa maisha yako.
Na hapo ndiyo unajua kwamba asili imelipa.

Matatizo mengi tunayoyapitia kwenye maisha yetu binafsi na hata matatizo ambayo dunia inapitia chanzo kikuu ni watu kwenda kinyume na kanuni za asili.
Uharibufu wa mazingira, ubovu wa vyakula na hata kutokuelewana baina ya jamii ni matokeo ya hatua ambazo tulichukua huko nyuma, ambazo zinakwenda kinyume na kanuni za asili.

Jukumu lako la kwanza ni kuzijua kanuni za asili, kisha kuishi kulingana na kanuni hizo.
Usishawishike kuvunja kanuni hizo, hata kama unajiambia ni kidogo kiasi gani, asili huwa haikopeshi, inalipa kamili na inalipa bila ya huruma.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuishi kulingana na kanuni za asili na siyo kushindana na asili.
#FuataKanuniZaAsili, #HuweziKuishindaAsili #MalipoNiHapaHapa

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1