“Let Fate find us prepared and active. Here is the great soul—the one who surrenders to Fate. The opposite is the weak and degenerate one, who struggles with and has a poor regard for the order of the world, and seeks to correct the faults of the gods rather than their own.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 107.12

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ambayo tumeiona leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KUWA NA MAANDALIZI…
Dunia haiendi kama tunavyopanga sisi, bali inaenda kwa mipango yake yenyewe.
Hivyo mara zote kuwa na maandalizi.
Jiandae kukutana na matokeo ambayo hukuyategemea.
Jiandae kukutana na magumu
Na jiandae kukutana na watu ambao watakuwa kikwazo kwako.
Huo ndiyo uhalisia wa dunia.

Changamoto kubwa ni kwamba wengi hufikiri wakishapanga basi dunia ina wajibu wa kuhakikisha wanapata walichopanga.
Wengi wanapokutana na matokeo tofauti na walivyopanga wanashangaa, kama vile ni kitu cha ajabu sana kutokea.
Wakati ni hali ya kawaida kabisa, ambayo ilipaswa kutegemewa na kuwa na maandalizi ya jinsi ya kuikabili.

Kama kitu chochote kinatokea kwenye maisha yako na ukapigwa na butwaa, ukajiambia hukutegemea kitokee, basi jua hukuwa na maandalizi.
Unapokuwa na maandalizi kwanza unakuwa tayari kupokea matokeo ambayo huyategemei na kutumia matokeo hayo kupiga hatua zaidi.

Usishindane na dunia,
Dunia huwa haikosei, hivyo unapopata matokeo ya tofauti, makosa ni yako.
Hivyo pia usikazane kuibadili dunia, ni kazi usiyoweza, badala yake kazana kubadilika wewe kwanza, ni kazi rahisi kwako.
Mara zote kuwa na maandalizi, na maisha yatakuwa rahisi kwako.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwa na maandalizi ya kutosha, ya kukuwezesha kupokea matokeo ya aina yoyote ile bila ya kushangazwa.
#KuwaNaMaandalizi #DuniaHaijaliKuhusuWewe #UtapataMatokeoUsiyotegemea

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1