Sisi binadamu huwa tunapenda kufikiri na kufanya maamuzi yetu kwa kutumia kingo mbili.

Tunapokubaliana na kitu basi tunakiona ndiyo kitu kizuri kabisa, kisichokuwa na kasoro yoyote. Na mtu yeyote anayetuambia kuna kasoro kwenye kitu hicho basi hajielewi au ana visa vyake.

Kadhalika tunapokuwa hatukubaliani na kitu basi tunakiona ni kibaya kabisa, kisichokuwa na manufaa yoyote. Kila tukiangalia kitu hicho tunaona ubaya na kasoro tu, na mtu mwingine anapoona kitu hicho ni kizuri basi tunamshangaa anaonaje uzuri kwenye kitu kama hicho.

Hili lipo sana kwenye mambo yanayohusisha hisia zaidi kuliko kufikiri. Mfano mapenzi, dini, siasa michezo na kadhalika. Lakini pia imekuwa inaingia kwenye ushirikiano wetu na wengine na hata yale tunayofanyia kazi.

Unapoleta mfumo huu wa kufikiri na kufanya maamuzi kwenye kingo mbili unajinyima fursa nyingi sana.

Kwenye maisha hakuna kitu chochote ambacho ni kizuri kabisa na kisichokuwa na kasoro yoyote. Na wala hakuna kitu ambacho ni kibaya kabisa na kisichokuwa na manufaa yoyote. Kila kitu kizuri kina mapungufu yake na kila kitu kibaya kina mazuri yake.

Kama wanavyosema, hata saa iliyosimama, huwa inasema muda wa kweli mara mbili kwa siku, hivyo ndivyo kila jambo linakwenda kwenye maisha.

Acha mara moja kufikiri kwenye kingo na angalia kitu kwa uhalisia wake, ona uzuri wa kitu lakini pia usijipe upofu wa mapungufu yake. Kadhalika kwenye vitu vyenye ubaya, usikimbilie kuona ubaya pekee, bali pia ona manufaa yake.

Tumia kila kitu kwa manufaa yaliyo ndani yake, hivyo usiwe mtu wa kukubaliana na kila kitu au kukataa kila kitu, bali tumia kile chenye manufaa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha