Kama huwezi kujivunia kwa kile unachofanya, kama huwezi kuwa na hamasa kubwa kwenye kile unachofanya na kuwa tayari kumshawishi yeyote anayehusika na kitu hicho akubaliane na wewe, basi unachofanya siyo sahihi kwako.

Inashangaza jinsi ambavyo watu wanafanya kazi au biashara ambazo hawawezi kujivunia nazo. Wakiwa mbele ya wengine hawathubutu kutaja aina ya kazi au biashara wanayofanya, kwa kuona wengine watawachukulia ni wa chini au wameshindwa.

Rafiki, chochote unachofanya, kina nafasi ya kukuwezesha wewe kufanikiwa zaidi. Lakini hutaweza kufanikiwa kama hutakuwa na hamasa kubwa kwenye kitu hicho. Kama huwezi kujivunia na kuwa tayari kusimama kifua mbele kwa wengine kuwaeleza kuhusu unachofanya, safari yako ya mafanikio itakuwa ngumu.

Rafiki, najua unajua kwamba kwenye haya maisha kila mmoja wetu anauza. Sasa mtu mmoja amewahi kusema kwamba mauzo ni mabadilishano ya hamasa. Akiwa na maana kwamba mtu mwenye kitu ambacho anauza, anakuwa na hamasa ya juu sana, ambayo anaiambukiza kwa yule anayenunua. Hivyo kama huna hamasa kubwa kwenye hicho unachofanya, huwezi kuwaambukia wengine hamasa na hivyo hawatanunua.

Jikubali wewe mwenyewe, jikubali kwa kile unachofanya na kuwa na hamasa kubwa kuhusu kitu hicho. Unapokutana na mtu yeyote ambaye kile unachofanya kinaweza kumsaidia basi unahakikisha habaki kama alivyokuwa awali, kabla hajakutana na wewe.

Na kama hupati hamasa hii kwenye kile unachofanya sasa, basi unachofanya siyo sahihi, kaa chini na ujitathmini upya na uje na kitu sahihi kwako kufanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha