Nimekuwa napata bahati ya kuwajua watu wengi tangu walipokuwa wanaanzia chini kabisa kwenye safari yao ya mafanikio mpaka pale wanapopiga hatua zaidi.
Na kwa kila ninayemjua ambaye ameanzia chini, wote mbeleni hukiri kwamba kabla hawajapiga hatua, walikuwa wanajizuia wao wenyewe.
Mtu mmoja alikuwa hajaanza biashara kwa miaka mingi, akisema mahali alipoajiriwa hawataki kabisa mfanyakazi awe na biashara nje ya ajira. Nikawa namsisitiza achague aina ya biashara ambayo haitaingiliana na kazi zake za ajira, baada ya kusua sua kwa muda mrefu, aliweza kuanzisha biashara na sasa inakwenda vizuri, huku akiendelea na kazi yake vizuri.
Mtu mwingine ambaye alikuwa hajaanza biashara kwa muda mrefu, alikuwa ananiambia ana mambo mengi inabidi ayakamilishe kwanza kabla hajaingia kwenye biashara. Nikawa namwambia mambo mengi aliyonayo hapaswi kuyaruhusu yamzuie kupiga hatua zaidi. Baada ya muda alikuja kuanza na mradi mdogo wa ufugaji wa kuku, na alipoanza kuokota mayai na kuuza, aliniambia nimeona kwa nini unasisitiza sana tuwe na biashara.
Na wengine wengi ambao nimekuwa nawashauri wajiunge na KISIMA CHA MAARIFA ili wajifunze zaidi, lakini wamekuwa na sababu mbalimbali, wengine ada, wengine wanasema hawana muda na kadhalika. Na wote nimekuwa nawasisitiza sana wajiunge, kwa sababu naijua thamani ya KISIMA. Ni mpaka pale mtu anapokuja kujiunga baadaye ndiyo anakiri kwamba amechelewa sana kujiunga.
Rafiki, kila mtu ana ukuta ambao unamtenga na mafanikio zaidi ya pale alipo sasa. Kwa wengine ukuta huo ni mkubwa, wengine ni mdogo, wengine hawana kabisa. Kadiri ukuta huo unavyokuwa mdogo, ndivyo mtu anavyokuwa na mafanikio makubwa.
Ukuta ninaouzungumzia hapa ni SABABU. Sababu yoyote unayojipa sasa kwamba huwezi kufanya, haiwezekani au inabidi usubiri, hicho ni kikwazo cha mafanikio yako. Kama kuna kitu unataka kufanya, lakini unajipa sababu yoyote ile kwa nini huwezi kufanya, unajichelewesha wewe mwenyewe kufanya.
Sisemi usiwe na sababu kabisa, ila ninachosema ni fanya licha ya kuwepo na sababu.
Mfano unataka kuanzisha biashara lakini huna mtaji, basi anza na biashara ambayo haihitaji mtaji au inaweza kuanza na mtaji kidogo.
Kwenye kila sababu unayojipa sasa, kuna fursa nyingi kabisa za kuanza, ni wewe kuchukua hatua na kuelekea kwenye mafanikio yako makubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
sababu ni kikwazo kikubwa sana hasa harakati za kujiletea maendeleo . kabla hujaikubali sababu ni lazima ujiulize mara tano au zaidi kweli hii sababu ni msingi? asante sana kocha kwa tafakari iliyo bora kabisa na ubarikiwe sana.
LikeLike
Kweli kabisa Kasanda,
Watu wengi wamekuwa wanakubaliana na sababu bila ya kuhoji kwa kina, na ndiyo maana wengi wanakwama.
LikeLike
Hii ni kweli kabisa, ukuta unaokutenga na mafanikio hasa ni sababu tunazojipa, ns pengine utayari wa kuwa tayari kwa lolote.
Binafsi naendelea kukushkru, tafakari ya Jana tarehe 25/07/2019 juu ya yule bwana kufanya kazi zaidi ya Massa 17 kuna kitu cha kujifunza zaidi ya pale.
LikeLike
Vizuri Beatus,
Tusikubali kabisa sababu ziwe kikwazo kwetu.
LikeLike