Ni kwa wewe kuwa mkubwa kwanza.

Huwezi kutatua tatizo ambalo limekuzidi ukubwa, litakutisha, kukupa hofu na kukukatisha tamaa.

Unapokutana na tatizo ambalo unaliona ni kubwa kwako, anza kwa kuwa mkubwa kuliko tatizo lenyewe.

Na ninaposema uwe mkubwa siyo kimwili badala yake kifikra. Anza kwa kuwa na mtazamo mkubwa kuliko tatizo ulilonalo. Anza kwa kuona mbali zaidi ya pale ulipo sasa. Anza kwa kujilazimisha kufikiri na kuvuka hisia ambazo zinakukwamisha kwenye matatizo unayokuwa nayo.

Unaweza kujijengea mtazamo huu mkubwa kuliko matatizo yanayokukabili kwa kusoma vitabu na kuangalia maisha ya wengine ambao wamepitia magumu lakini wakayavuka.

Kwa kutumia vizuri rasilimali hizo mbili, hakuna tatizo lolote linaloweza kuwa kubwa kwako, kukutisha au kukupa hofu. Utaweza kujiamini kwa kila unachopitia kwenye maisha yako, kwa kujua utaipata njia na kama haipo basi utaitengeneza njia.

Hebu rudia kauli hii ambayo itakupa nguvu leo; “kwa tatizo hili nililonalo, nitapata njia ya kulitatua na kama haipo basi nitatengeneza njia hiyo.”

Nenda kaishi hivyo leo na kila siku ya maisha yako, na hakuna tatizo litakalokuzidi ukubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha