Nimekuwa nasema kitu kimoja, kama hutapata sehemu yoyote ya kujifunza kuhusu misingi ya mafanikio, basi angalia sheria za asili. Angalia jinsi wanyama na mimea inavyoishi na kuendesha maisha yao hapa duniani na futa misingi hiyo, kwa hakika utafanikiwa.

Kuna mfano mmoja umekuwa unatumiwa sana kuhusu nguvu ya uvumilivu, kuhusu mti wa mbuyu. Kwamba mbegu ya mbuyu inapopandwa, inachukua miaka mpaka mche ujitokeze, lakini mche ukishatoka unakua kwa haraka sana.

Kila kitu kina muda wake, licha ya kuweka juhudi kubwa na kila unachopaswa kuweka, bado huwezi kulazimisha muda wa kitu kutokea.

Mtu mmoja amewahi kusema huwezi kupata mtoto kwa mwezi mmoja kwa kuwapa wanawake tisa ujauzito mmoja. Kwamba kwa sababu mimba inachukua miezi tisa, huwezi kugawa miezi hiyo kwa wanawake tisa ili upate mtoto ndani ya mwezi mmoja.

Hivyo rafiki, weka juhudi kubwa sana, ifanye kazi yako, hakikisha kila unachopaswa kufanya unafanya.

Halafu sasa, ukishafanya, unapaswa kuwa na subira, unapaswa kuupa muda nafasi yake, unapaswa kuipa asili nafasi ya kufanya kazi yake. Usiwe na papara, wengi wameharibu mafanikio yao makubwa kwa kukosa subira.

Kumbuka kwenye mafanikio hakuna kuchelewa wala kuwahi, bali kuna wakati sahihi wa kila jambo sahihi.

Fanyia kazi jukumu lako ambalo ni kuweka juhudi na kuzalisha matokeo bora kabisa, na kisha acha muda na asili vifanye kazi yake ya kukulipa wewe kulingana na ulivyotoa. Utafika wakati sahihi wa wewe kupata unachotaka, kama tu utaendelea kufanya kilicho sahihi bila ya kukata tamaa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha