Kama unajiambia huna muda wa kufanya kitu, nina habari njema kwako, tatizo lako siyo muda, tatizo lako ni umuhimu ambao umeweka kwenye kitu hicho.

Labda nikupe mfano. Una gari yako, ambayo ina uwezo wa kubeba gumia 10 pekee, na huwezi kuongeza zaidi ya hapo. Umeenda sokoni kununua vitu ili ukaviuze sehemu nyingine, na ukanunua gunia 10 za mchele. Gari yako tayari imeshajaa. Wakati unataka kuondoka, anakuja mtu kwako ana gunia moja la dhahabu anauza kwa bei rahisi sana kwa sababu anataka fedha haraka na wengi wanashindwa kununua. Wewe una fedha, lakini gari yako haina nafasi, je unafanya nini?

Je utasema siwezi kununua dhahabu hii kwa sababu tayari gari imejaa mchele? Nafikiri hilo siyo swali, hutafikiria hata mara mbili, utanunua dhahabu, utapunguza mchele ili upate nafasi ya kuweka dhahabu. Hivyo basi, gari ambayo tayari ilikuwa umeshajaa, kilipokuja kitu ambacho ni bora zaidi, nafasi imepatikana.

Hivyo ndivyo maisha yako yalivyo, hasa kwenye muda. Kwa sasa muda wako umejaa, kwa hakika huna muda, mambo ya kufanya ni mengi na muda ulionao ni mchache. Hivyo basi, unapopata wazo la kufanya kitu kingine kipya, hakuna muda zaidi unaoweza kuutengeneza, badala yake unahitaji kuacha kufanya baadhi ya vitu unavyofanya sasa.

Unahitaji kuangalia kile kipya unachotaka kufanya, ukilinganisha na vile vya zamani ambavyo umekuwa unafanya, je kipi cha thamani na muhimu zaidi.

Chukua mfano unataka kujenga tabia ya kujisomea vitabu, lakini unajiambia huna muda. Hebu kaa chini na orodhesha jinsi unavyotumia muda wako wa siku nzima, na kisha jiulize je yote unayofanya ni muhimu kuliko kujifunza? Kama unatumia muda wako kutembelea mitandao ya kijamii, jiulize je kutembelea mitandao ya kijamii ni bora kuliko kusoma vitabu?

Ukishaanza kupima vitu kwa thamani na ubora wake, utapata muda na nafasi ya yale ambayo ni muhimu zaidi. Lakini kama hutafanya tathmini hiyo, utazikosa fursa za kupiga hatua zaidi kwa kisingizio kwamba huna muda, kumbe muda unao ila unautumia vibaya.

Kila wakati unapojiambia huwezi kufanya kitu kwa sababu huna muda, jikamate hapo hapo na fanya tathmini ya matumizi ya muda wako. Hili litakufanya uone jinsi unavyopoteza muda wako na kuweza kupangilia vizuri matumizi ya muda wako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha