Uzembe ni moja ya vikwazo vikubwa kwenye mafanikio ya wengi.
Na uzembe umekuwa unatengenezwa kidogo kidogo, kwa kukosa umakini kwenye ufuatiliaji wa kile kitu ambacho mtu unafanya.
Kwa kila kitu unachofanya, unapaswa kuwa mfuatiliaji kwa undani, usiishie juu juu, chimba ndani zaidi, pata taarifa zaidi na jua kila kitu unachopaswa kujua.
Hili ni muhimu sana kwenye biashara, hasa pale unapokuwa umeajiri watu wengine wakusaidie.
Watu hao watajituma kadiri wewe unavyowafuatilia.
Wakijifunza kwamba wewe siyo mfuatiliaji kwa undani, kwamba unaamini chochote unachoambiwa kama ndiyo kitu sahihi, kidogo kidogo wanaanza kujifunza kukudanganya. Hili linaendelea kukua mpaka inafika hatua unachoambiwa ni uongo tu.
Lakini watu hao wanapojifunza kwamba unafuatilia kila kitu, unadhibitisha kila unachoambiwa, wanalazimika kuwa wa kweli, wanalazimika kusema kilicho sahihi kwa sababu wanajua utafuatilia.
Hivyo ndivyo unavyopaswa kufanya kwenye mambo yako yote, kuwa na umakini wa hali ya juu, kufuatilia kwa undani na kutokuruhusu uzembe uingie kwa namna yoyote ile.
Matatizo mengi tunayopitia kwenye maisha huwa yanaanzia kwenye uzembe na chanzo kikuu ni kukosa umakini kwenye kile ambacho mtu anafanya. Weka umakini zaidi, fuatilia kwa undani kila kitu na uzembe utapungua pamoja na changamoto zinazotokana na uzembe huo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,