“Philosophy isn’t a parlor trick or made for show. It’s not concerned with words, but with facts. It’s not employed for some pleasure before the day is spent, or to relieve the uneasiness of our leisure. It shapes and builds up the soul, it gives order to l ife, guides action, shows what should and shouldn’t be done—it sits at the rudder steering our course as we vacillate in uncertainties. Without it, no one can live without fear or free from care. Countless things happen every hour that require advice, and such advice is to be sought out in philosophy.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 16.3
Nani anayeweza kusema ameiona siku hii ya leo kwa nguvu na akili zake mwenye? Ni mpumbavu pekee.
Werevu wote wanajua nafasi hii tuliyoipata leo ni kwa bahati tu, siyo kwa nguvu au akili zetu, na wala siyo kwa sababu tunastahili sana.
Tumeipata nafasi hii kwa sababu kazi yetu hapa duniani bado haijaisha, hivyo siku ya leo badala ya kwenda kuipoteza kwa mambo yasiyo muhimu, tuitumie vyema, kwa sababu hatuna uhakika kama tutapata siku nyingine kama hii.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari SIYO KWA AJILI YA MAONESHO, NI KWA AJILI YA MAISHA BORA….
Chochote unachofanya kwenye maisha yako, usifanye kwa sababu unataka uonekane unafanya, wala usifanye kwa sababu kila mtu anafanya, bali fanua kwa sababu kitaboresha maisha yako na ya wengine pia.
Ubora wa maisha ndiyo kipimo sahihi kwako kwenye mambo unayofanya, usiwe mtu wa kusukumwa na kutaka kuonekana au kufuata mkumbo.
Tukianzia kwenye kazi au biashara unayofanya, sababu kuu ya wewe kuwa kwenye kazi au biashara hiyo inapaswa kuwa ni ubora wa maisha unaopata wewe na wengine pia. Na siyo mwonekano au cheo unachopata.
Tukienda kwenye falsafa na dini, sababu kuu ya wewe kuwa kwenye falsafa au dini yoyote inapaswa kuwa ule msingi sahihi unaopata wa kuendesha maisha yako, ambao unakuwezesha kukabiliana na changamoto na kusimama imara.
Usiingie kwenye falsafa au dini kwa sababu ndiyo umezoea hivyo, au unataka ukubalike na wengine, au kwa sababu ndiyo umezaliwa na kulelewa hivyo.
Usifanye chochote kwa ajili ya maonesho, badala yake fanya kwa ajili ya maisha bora, na kwa hakika utapiga hatua sana kwenye maisha yako.
Kwa bahati mbaya tunaishi kwenye zama ambazo maonesho yanapewa kipaumbele kuliko ubora wa maisha.
Zama ambazo kila mtu anataka kuonekana, kila mtu anataka kuwa na maoni na yasikike na kila mtu anaweza kuchangia kwenye kitu chochote.
Hizi ni zama hatari, ambapo kama huna msingi sahihi, maonesho yatakupoteza. Utajikuta unakazana sana, lakini hupigi hatua na wala ndani yako huridhiki, kwa sababu ndani yako huwi bora, licha ya nje kuonekana.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kufanya yale ambayo yanakupa maisha bora na siyo yale ambayo yanaleta maonesho pekee. Mwisho wa siku hakuna atakayekumbuka maonesho yako, lakini kama hutakuwa bora, hilo litakuumiza maisha yako yote.
#IshiMaishaYako #FanyaKilichoSahihi #TafutaUboraSiyoMaonesho
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1