Ushauri ni moja ya vitu ambavyo vimekuwa vinatolewa kwa urahisi sana, kila mtu amekuwa na uwezo wa kutoa ushauri kwa wengine.
Ukuaji wa mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii umefanya kila mtu aweze kutoa maoni yake kwenye jambo lolote lile, na hili pia limechangia kila mtu kuweza kuwa mshauri.
Kuna wakati tunakutana na ushauri wa aina mbalimbali, na tunajikuta njia panda, tusijue kama ni ushauri sahihi kwetu kuchukua na kufanyia kazi.
Mimi Kocha wako, leo nakwenda kukuonesha watu ambao hupaswi kuchukua ushauri wao kabisa, au kama utauchukua basi iwe kwa tahadhari sana.
Moja; watu wanaokupa ushauri wa bure. Hawa ni wale wanaokuambia ushauri wangu wa bure ni huu … Hakuna kitu chenye gharama kama ushauri wa bure. Utafurahia kuupokea bure, lakini utakapoanza kuutumia ndiyo utajua gharama yake.
Mbili; watu wanaokupa ushauri kabla hujawaomba. Anajitokeza mtu na kuanza kukupa ushauri kwenye jambo unalofanya au unalopitia, kabla hata hujawaomba ushauri. Ushauri wanaokupa hauwezi kuwa sahihi, kwa sababu hawajui kwa undani nini unapitia. Kuna mambo watakuwa wanayaona kwa nje, ila kwa ndani hawajui, mpaka pale utakapowaeleza. Hivyo ushauri unaotoka kwa watu ambao hujawaomba, ni ushauri usio sahihi.
Tatu; ushauri kutoka kwa wasiofanya wanachoshauri. Ni vyema kupata ushauri kutoka kwa yule anayefanya kile anachoshauri au anayeelekea huko. Kama mtu hana ujuzi au uzoefu kwenye jambo fulani, basi ushauri wake uchukue kwa tahadhari kubwa, kwa sababu utakuwa ni ushauri wa kuokota okota na usio na uhakika.
Nne; ushauri kutoka kwa watu waliokutana na bahati. Labda ameshinda bahati nasibu au kamari. Ushauri wowote anaokupa hautakufaa. Huwezi kurudia bahati mara mbili. Hata yeye mwenyewe akifuata ushauri anaokupa hawezi kupata bahati hiyo tena.
Tano; mtu ambaye hataathirika na ushauri anaokupa. Mwandishi Nasim Talib anaita SKIN IN THE GAME. Kwamba kama mtu haathiriki na matokeo yanayotokea, basi kuwa na tahadhari sana na ushauri anaokupa. Au kama mtu ananufaika na matokeo yoyote yatakayotokea, kuwa makini.
Ukiwa makini katika kuchagua aina gani ya ushauri unaopokea na kufanyia kazi, hasa kwa kuwachagua watu sahihi wa kukushauri, kuwaeleza kwa kina hali unazopitia na kisha kuwahoji kwenye kila wanachokushauri, utaweza kupata ushauri bora sana utakaokuwezesha kuvuka changamoto mbalimbali unazopitia kwenye maisha yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ahsante kocha
LikeLike
👍
LikeLike