Hatufanyi kazi iliyo bora kabisa kwa sababu hatuweki akili yetu na umakini wetu wote kwenye kile tunachofanya.

Hatumalizi kazi tulizonazo kwa wakati kwa sababu tunaruhusu usumbufu wa kila aina kuingilia kazi zetu.

Dawa ya kuondokana na hali hizo ni kutukuza kile unachofanya.

Na hapa nina maana rahisi sana, wala usije ukaanza kufikiria unawezaje kutukuza unachofanya.

Unachofanya ni kupanga kufanya kitu, halafu kwa muda huo uliopanga kufanya kitu hicho, hufikirii kitu kingine chochote bali tu kile unachofanya. Fikra zako zote, nguvu zako zote na umakini wako wote unapaswa kwenda kwenye kile unachofanya. Usipoteze hata sekunde moja kuhangaika na kisichohusika na kile ulichopanga kufanya.

Kwa mara ya kwanza linaweza kuwa zoezi gumu, kwa sababu najua usumbufu unaokuzunguka ni mwingi, kuanzia ndani yako na hata nje. Lakini unapolifanya kuwa zoezi unalolirudia kila wakati, unazidi kuimarika na kunufaika zaidi.

Mfano, anza na dakika kumi za kufanya kitu kimoja bila ya kuruhusu usumbufu wowote ule, simu iweke kwenye hali ya utulivu kiasi kwamba hata kama itaita hutaisikia kabisa (hakuna dharura yoyote ambayo haiwezi kusubiri dakika kumi). Ukifaulu dakika kumi nenda 20, kisha 30, kisha saa moja na kuendelea.

Kadiri unavyoweza kuweka utulivu kwenye kile unachokifanya kwa muda mrefu, ndivyo unavyonufaika zaidi. Anza hili leo na ufanye huu kuwa utaratibu wa maisha yako ya kila siku. Utaona maana ya kile unachofanya, lakini pia utamaliza majukumu yako kwa wakati na ubora wa hali ya juu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha