Hakuna kitu kisichokuwa na manufaa kwenye maisha yetu.

Hata kama kitu ni kibaya kiasi gani, kuna namna tunaweza kukitumia na kikaleta manufaa kwenye maisha yetu.

Tabia ya kuahirisha mambo imekuwa kikwazo kwa watu wengi kupiga hatua na kufanikiwa kwenye maisha yao. Unakuwa na malengo makubwa na unapanga kabisa hatua za kuchukua, lakini inapofika wakati wa kuchukua hatua hizo, unaahirisha, unajiambia utafanya kesho. Cha kushangaza kesho hiyo huwa haifiki, na hivyo mtu anashindwa kabisa kupiga hatua.

Sasa pamoja na madhara ya tabia hii ya kuahirisha mambo, bado kuna namna tunaweza kuitumia kwa manufaa makubwa kwetu.

Na sehemu nzuri tunapoweza kutumia tabia hii ni kwenye kukata tamaa au kuacha kufanya kitu. Katika safari yetu ya mafanikio, kuna wakati tunakutana na mambo magumu ambayo yanatukatisha tamaa. Tunafika mahali na kujiambia hatuwezi kuendelea tena, bora tuishie hapo. Kuishia njiani hivi hakuna manufaa yoyote kwako.

Ili kuondoana na tabia hiyo ya kukata tamaa na kuacha kufanya mambo, tumia tabia ya kuahirisha mambo. Kama unajiambia leo ndiyo mwisho wa kufanya, jiambie hutatekeleza hilo leo, bali kesho. Yaani ahirisha mpango wako wa kuacha kile ambacho unataka kuacha. Jiambie leo utafanya kwa ubora wako wote, lakini kesho utaacha.

Na inapofika kesho mchezo huo unaendelea, jiambie kesho ndiyo utaacha. Unaendelea kujiambia kesho hivyo mpaka unakuta umevuka ugumu uliokuwa unakutisha au kukukatisha tamaa.

Ukiweza kuitumia tabia ya kuahirisha mambo kwenye kuahirisha kukata tamaa na kuacha, utakuwa king’ang’anizi mkubwa na kuweza kupiga hatua kubwa licha ya magumu unayokuwa umepitia.

Ahirisha kukata tamaa na kuacha kufanya leo na weka nguvu zako zote kwenye kile unachotaka kuacha kufanya, kama vile ndiyo siku yako ya mwisho kukifanya. Kesho rudia tena hiyo na kila siku mpya unayoianza iishi hivyo, haitakuchukua muda utaanza kuvuna matokeo mazuri.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha