Siku hizi kila mtu anataka kuwa maarufu.

Na umaarufu wenyewe sasa unachekesha sana.

Kwa sababu ni umaarufu hewa, umaarufu ambao hauna msingi, umaarufu ambao upepo ukivuma tofauti basi unapotezwa kabisa.

Tunapenda umaarufu kwa sababu tunajua utatupa ‘koneksheni’, utatufungulia baadhi ya milango kwa sababu unapokuwa unajulikana ni rahisi kupata baadhi ya vitu kuliko ukiwa hujulikani.

Lakini sasa, umaarufu ambao wengi wanafanyia kazi ni umaarufu hewa, au kama wengi wanavyouita ‘kiki’, mtu anakazana kupata jina kubwa kwa kufanya mambo yasiyo na maana.

Kwenye zama hizi za mitandao ya kijamii, wengi pia wameweka nguvu zao kutafuta umaarufu wa mtandaoni, kwa kuhangaika kupata wafuasi wengi mtandaoni, huku wakiwa hawana kitu cha msingi cha kuwapa wafuasi hao ili waendelee kuwa pamoja.

Ili kutuliza kiu na njaa ya wafuasi hao, ambao wanataka sana kusikia kwa yule wanayemfuata, wengi wanalazimika kufanya mambo ya ajabu ili tu waonekane nao pia wapo.

Rafiki yangu mpendwa, unajua jinsi ninavyokupenda na jinsi nilivyoyatoa maisha yangu kuhakikisha wewe unakuwa na maisha bora.

Leo nakupa njia moja ya uhakika ya kujijengea umaarufu sahihi, umaarufu unaodumu mara zote. Njia hiyo ina hatua mbili;

Hatua ya kwanza ni kufanya kitu cha tofauti, kitu bora na chenye manufaa kwa wengine. Hapa ndipo unapojitofautisha wewe na watu wengine wote, hapa ndipo unapoweka msingi wako, ambao unawafanya watu waje kwako, kwa sababu una kitu ambacho wanakihitaji.

Hatua ya pili ni kusambaza kile unachofanya kwa wengine, hapa sasa ndiyo unahakikisha kwamba kile unachofanya, kinawafikia watu wote unaowalenga, wale ambao wanaweza kunufaika nacho.

Ukichukua hatua hizi mbili, utakuwa sumaku ambayo inawavuta watu sahihi kuja kwako. Hutahitaji kupiga kelele, hutahitaji kufanya mambo ya ajabu, watu watakuja kwako kwa sababu una kitu muhimu wanachohitaji, na hawatakuja wenyewe, watakuja na wenzao pia.

Chagua ni kipi cha tofauti unachofanya kwenye maisha yako, ambacho unataka kikusimamishe na kukutofautisha na wengine, kisha kifanye kwa ubora wa hali ya juu sana, na kisambaze kwa wale kinaowagusa, na ni swala la muda tu, utakuwa maarufu na mtandao wako utakuwa mkubwa sana.

Acha wasioelewa wahangaike na kiki ambazo hazidumu, wewe kazana kutoa thamani kubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha