Unaweza kuwa unakazana sana kuwasaidia watu, lakini huoni matokeo mazuri. Hilo linaweza kukushangaza usielewe kwa nini mtu apinge msaada ambao unampa kwa kujitoa zaidi wewe.

Unachopaswa kujua ni kwamba kuna watu ambao hawasaidiki, hata ufanye nini. Hivyo ni muhimu kuwajua mapema kabla hujapoteza muda, nguvu na hata fedha zako kuwasaidia watu hao.

Ni vigumu sana kumsaidia mtu ambaye anafikiri hana tatizo. Kama mtu anaamini hana tatizo, utamsaidia nini? Haijalishi utafanya nini, kwake haitakuwa na maana kwa sababu anaamini hana tatizo, na hivyo hahitaji msaada wowote.

Ni vigumu zaidi kumsaidia mtu ambaye anafikiri watu wengine ndiyo wenye matatizo. Kama mtu anaamini matatizo anayopitia yeye ni kwa sababu ya watu wengine, itakuwa vigumu sana kwako kuweza kuwasaidia. Kwa sababu wanaamini wao hawana shida, ila watu wengine ndiyo wenye shida.

Hivyo kabla hujaanza juhudi za kumsaidia mtu, elewa kwanza yupo upande gani wa tatizo. Je anakubali kwamba ana tatizo? Na je anajua yeye amechangia kwenye tatizo alilonalo? Kama majibu ni ndiyo basi huyo ni mtu ambaye mnaweza kufanya kazi pamoja. Lakini kama majibu ni hapana, okoa muda na nguvu zako kwa kufanya mambo mengine ya msingi.

Linaloendana na hilo ni kumpa mtu ushauri ambao hajakuomba, nako ni kupoteza muda, kwa sababu hataufanyia kazi. Hata kama mtu anaonekana anaweza kutoka pale alipokwama kwa ujuzi au uzoefu unaoweza kumpa, kama hajaridhia yeye mwenyewe kwamba anahitaji ushauri, ataona ushauri wako kama usumbufu tu kwake.

Unaweza kuwa na nia nzuri sana ya kuwasaidia wengine, lakini jua kuna watu ambao hawasaidiki, hata ufanye nini. Kuwajua mapema kutaokoa muda wako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha