Huwa tunakuana na fursa mbalimbali kwenye maisha yetu.
Ili kuchagua ni fursa ipi mtu utaifanyia kazi, watu wamekuwa na vigezo mbalimbali wanavyotumia.
Na wengi hutumia kigezo cha malipo, huwa wanachagua ile fursa ambayo inawalipa zaidi, kitu ambacho siyo kibaya kwa sababu nani asiyependa fedha?
Lakini katika kuchagua kile kinacholipa zaidi, watu huwa wanaangalia zaidi leo na siyo kesho. Hivyo wanafurahia kupata kiasi kidogo cha fedha leo na siyo kupata kiasi kikubwa zaidi baadaye.
Kigezo bora cha kuchagua fursa, siyo malipo, bali kujifunza.
Yaani usichague fursa kwa sababu inakulipa zaidi sasa, bali chagua fursa kwa sababu inakupa nafasi ya kujifunza zaidi.
Sasa unapojifunza zaidi, unajitengenezea nafasi ya kufanya makubwa zaidi baadaye na hivyo kuongeza kipato chako zaidi.
Uwekezaji muhimu na bora kabisa kuufanya kwenye maisha yako ni uwekezaji wa ndani yako mwenyewe. Hivyo unapojifunza zaidi, unajitengenezea uwezo wa kuingiza kipato kikubwa zaidi na hilo linakuwa na manufaa makubwa zaidi.
Usiwe unachagua fursa kwa kigezo cha malipo pekee, bali tanguliza kigezo cha kujifunza. Kama ipo nafasi ya kujifunza, hata kama malipo ni kidogo, kile unachojifunza kitakuwa na manufaa makubwa kwako baadaye.
Kila fursa unayoingia, anza kwa kujiuliza nakwenda kujifunza nini, badala ya kujiuliza nakwenda kuingiza kiasi gani.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,