Maji ndiyo kitu huru kuliko vyote hapa duniani.
Hii ni kwa sababu hakuna chochote kinachoweza kuyazuia maji.
Yakiwekwa kwenye kikombe yanaingia, yakiwekwa kwenye chupa yanaingia.
Yanaweza kuwa yabisi, yakawa kimiminika na yakawa mvuke kulingana na mazingira yanavyotaka.
Yanaweza kuchukua umbo na nafasi yoyote inayopatikana.
Yanaweza kuvunja miamba mikubwa sana hata kama ni kwa tone moja moja.
Kama unataka kuwa na mafanikio makubwa na yenye uhuru kwenye maisha yako, basi kuwa kama maji.
Kuwa tayari kubadilika pale mazingira yanapokutaka ubadilike,
Usilazimishe mambo yaende kama unavyotaka wewe, bali wewe nenda na namna mambo yanavyokwenda.
Pia kuwa king’ang’anizi sana kwenye chochote unachofanya, na nguvu hiyo ya ung’ang’anizi itakuwezesha kufanya makubwa kama matone ya maji yanavyovunja mwamba mkubwa.
Kila unapokutana na ugumu kwenye maisha yako, jiulize kama ungekuwa maji ungekabilianaje na ugumu huo. Pata picha ya maji yangu yanatoka kwenye chemchem, yanapita kwenye mifereji, vijito, mito mpaka kufika baharini au ziwani. Pia pata picha maji hayo yanabadilika kuwa mvuke na kutengeneza mvua. Kisha jiulize ni mabadiliko gani unayohitaji pale ulipokwama sasa na kuweza kuendelea.
Ukiwa tayari kubadilika, mambo yako yatakwenda vizuri sana. Ukipingana na mabadiliko, mambo yako yatakuwa magumu sana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Hakika hii nzuri sana, nimeipenda ya kuwa kama maji. Maisha yanataka mtu mbishi, kung’ang’ana, anaethubu, anaefanya mambo mengi.
LikeLike