#TANO ZA JUMA #35 2019; Kuwa Kawaida Au Kuwa Huru, Mwongozo Wa Kutengeneza Uhuru Kamili Wa Maisha Yako, Hatua Tano Za Kutoka Kwenye Ajira Mpaka Kujiajiri, Jinsi Ya Kuondoka Kwenye Madeni Yanayokutesa Na Kupunguza Uhalifu, Watu Wanapaswa Kujiajiri.

Hongera sana mwanamafanikio kwa juma la 35 ambalo tumeweza kulimaliza vyema.

Ni imani yangu kwamba juma hilo limekuwa bora sana kwako, umeweza kujifunza na kuchukua hatua kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

Nichukue nafasi hii kukukaribisha kwenye TANO ZA JUMA la 35 la mwaka huu 2019. Kwenye juma hili tunakwenda kujifunza jinsi ambavyo mtu unaweza kutengeneza uhuru kamili wa maisha yako kupitia kujiajiri wewe mwenyewe badala ya kutegemea ajira pekee.

Tunakwenda kujifunza hilo kupitia kitabu kinachoitwa Freelance to Freedom: The Roadmap for Creating a Side Business to Achieve Financial, Time and Life Freedom kilichoandikwa na mpiga picha aliyeweza kutoka kwenye ajira mpaka kujiajiri mwenyewe na kufikia mafanikio makubwa. Mpiga picha huyo ni  Vincent Pugliese akishirikiana na mke wake Elizabeth katika safari ya kutoka kwenye utumwa wa ajira pamoja na madeni mpaka kufikia uhuru wa kifedha, muda na hata maisha kwa ujumla.

freelance to freedom

Najua unasoma hapa kwa sababu unataka uhuru kwenye maisha yako, na zipo njia sahihi kwako kufikia uhuru huo, iwe umeajiriwa au kujiajiri mwenyewe. Soma makala hii ya TANO ZA JUMA, chukua hatua na maisha yako hayatabaki pale yalipo sasa.

#1 NENO LA JUMA; KUWA KAWAIDA AU KUWA HURU.

Kwenye maisha unaweza kuchagua upande mmoja kati ya pande hivi mbili. Unaweza kuchagua kuwa mtu wa kawaida au kuchagua kuwa mtu huru. Ukichagua kuwa mtu wa kawaida maana yake unapoteza uhuru wako. Na ukichagua kuwa huru maana yake unaacha kuwa kawaida. Huwezi kuwa mtu wa kawaida na huru kwa wakati mmoja, hicho hakipo kabisa.

Nifafanue kwa kina hapa ili tuelewane vizuri.

Hawa ndiyo watu wa kawaida kwenye jamii zetu, ambao wameajiriwa kwenye kazi ambazo hawazipendi, ila wanataka kipato. Kipato wanachopata hakiwatoshelezi, hivyo wanaingia kwenye mikopo. Hapo sasa wanakuwa wamekwama kwenye ajira na madeni kwa wakati mmoja. Maisha yao yanakwenda hivyo mpaka wanapostaafu na kuishia kuwa na maisha magumu.

Watu hawa wa kawaida wapo kwenye kila shughuli ya kijamii, ni mashabiki wa kila mchezo, watembeleaji wazuri wa kila mtandao wa kijamii, washiriki wa kila sherehe, waaminifu kwenye starehe na mapumziko ya kila mara.

Watu wa kawaida wanafanya kile ambacho kila mtu anafanya, na hivyo kwa wingi wao, wanaishia kuwa na maisha magumu na yasiyo na uhuru.

Hizo ndizo sifa za mtu wa kawaida, sasa tuangalie sifa za mtu huru.

Mtu huru anafanya kile anachotaka kufanya, kwa muda ambao anataka kukifanya na hasukumwi na fedha. Mtu huru ana uhakika wa maisha yake kwenda iwe ana kipato cha moja kwa moja au la.

Mtu aliye huru akianzia kwenye ajira anakuwa na biashara yake ya pembeni ambayo anaiwekea nguvu kubwa ili ikue na kumwongezea kipato. Mtu huyu hana muda wa kupoteza kwenye mambo yasiyo na tija, kila wakati yupo kwenye kazi au mambo muhimu zaidi kwake.

Mtu aliye huru hana mkopo wowote ambao amechukua kwa jina lake na kuweka mali zake binafsi rehani. Magari, nyumba na mali nyingine anazomiliki amenunua kwa fedha taslimu au kama alichukua kwa mkopo ameshalipa wote. Ikitokea mtu huyu ana mkopo, basi unakuwa ni kwa jina la biashara na hivyo hauna hatari yoyote kwa mali zake binafsi.

Mtu aliye huru hapatikani kila mahali na kwa urahisi, hana marafiki wengi na hajali sana wengine wanamfikiriaje.

Mtu aliye huru anaongoza kwa kusemwa vibaya, kukosolewa na kupingwa kwa chochote anachosimamia au kuishi. Anaonekana ni mtu asiyejua kuishi maisha kama wengine au asiyejali kuhusu wengine.

Lakini ni mtu aliye huru anayekuja kuwa na mchango mkubwa na bora sana wa jamii nzima, ni mtu pekee anayekuwa na maisha tulivu na yenye furaha.

Nirudie tena swali, unataka kuwa mtu wa kawaida au mtu huru?

Kama unataka kuwa mtu wa kawaida unaweza kuishia kusoma hapa, usiendelee maana yanayofuata hayatakufaa.

Lakini kama unataka kuwa huru, basi karibu sana, yanayofuata hapa ni mafunzo sahihi kwako kuelekea kwenye uhuru wako.

#2 KITABU CHA JUMA; MWONGOZO WA KUTENGENEZA UHURU KAMILI WA MAISHA YAKO.

Vincent Pugliese ambaye alikuwa mpiga picha aliyeajiriwa kwenye jarida la michezo, aliyaanza maisha yake kama watu wengine wanavyoanza maisha yao. Kwa kununua vitu vingi kwa mkopo na sehemu kubwa ya mshahara wake kwenda kulipa mkopo huo. Hali hiyo ilipelekea maisha yake kuwa magumu sana kitu ambacho hakukifurahia.

Aliamua kuchukua hatua ya kutafuta uhuru wa maisha yake baada ya kukutana na kitabu kinachofundisha kuhusu uhuru wa kifedha. Kwenye kitabu chake kinachoitwa FREELANCE TO FREEDOM, Vicent anatushirikisha safari nzima ya maisha yake ya kutoka kwenye utumwa mpaka kwenye uhuru.

Hapa tunakwenda kujifunza yale muhimu ambayo Vicent ametushirikisha, ambayo hata sisi tukiyafanyia kazi basi tunaweza kuondoka kwenye utumwa na kwenda kwenye uhuru.

Karibu sana tujifunze na kuchukua hatua kuelekea kwenye uhuru wa maisha yetu.

  1. Tumekuwa tunadanganywa sana tangu tukiwa watoto. Kwamba njia pekee ya kufanikiwa kwenye maisha ni kusoma kwa bidii, kufaulu sana na kisha kupata kazi yenye malipo mazuri, ambayo tutaifanya mpaka kustaafu kwetu na hapo tutalipwa mafao mazuri. Ushauri huu kwa zama hizi haufanyi tena kazi, uhakika wa kazi umekuwa mdogo na hata unapoipata, kipato hakitoshelezi kuendesha maisha. Hivyo tunahitaji ushauri sahihi kwa sasa ambao ni mtu kuwa na njia ya kuingiza kipato ambayo haina ukomo, kwa kujiajiri mwenyewe hata kama upo kwenye ajira.
  2. Lengo la ajira siyo wewe kuitegemea kwa maisha yako yote, lengo la ajira ni wewe kupata mahali pa kuanzia kutengeneza uhuru wako wa kifedha. Hakuna ubaya wowote kwenye kuajiriwa, ubaya unakuja pale unapoitegemea ajira pekee kama ndiyo chanzo chako kikuu cha kukuingizia kipato maisha yako yote. Ajira pekee haiwezi kutekeleza hilo, hivyo unapaswa kutumia ajira kama ngazi ya kuenda mbele zaidi ambapo ni kujiajiri.
  3. Faida za kujiajiri mwenyewe ni nyingi, haziishii tu kwenye kutengeneza kipato chako kwa uhuru, bali pia zinakwenda kwenye kufanya kitu ambacho unakipenda na chenye maana kwako. Mara nyingi watu wanapoajiriwa wanalazimika kufanya kazi ambayo hawaipendi au haina maana kwao. Lakini unapojiajiri unakuwa huru kuchagua kufanya kile ambacho unapenda kufanya na chenye maana kubwa kwako binafsi.
  4. Muda haukusubiri wewe uwe tayari kuanza. Wakati sahihi kwako kutengeneza uhuru wa kifedha ulikuwa siku unayoanza kabisa kazi, lakini kama umechelewa na hukuweza kuanza kipindi hicho, basi wakati mwingine mzuri kwako ni sasa. Anza leo kutengeneza uhuru wa maisha yako kwa kufanya kile ambacho unapenda kufanya na kutoa thamani kubwa kwa wengine ambao watakuwa tayari kukulipa wewe.
  5. Vijana wengi kwa sasa wanayaanza maisha yao wakiwa na deni kubwa la elimu ya juu, huku wakiwa hawana uhakika wa kupata ajira. Kama vijana hawa wangeshauriwa vizuri, muda ambao wameutumia chuoni kusoma kitu ambacho hakina uhakika wa ajira, na kuweka muda huo kwenye kutengeneza biashara inayotokana na kitu wanachopenda kufanya, wakati ambao wenzao wanamaliza chuo wakiwa na madeni, wao wanakuwa wameshafika mbali sana kibiashara na hawana deni kabisa.
  6. Dunia inazidi kudhihirisha kwamba hadithi ya nenda shule, soma kwa bidii, faulu na utapata kazi nzuri imeshapitwa na wakati. Kwa sasa makampuni makubwa kabisa yameshaweka wazi kwamba elimu siyo kigezo chao kikuu kwenye kuajiri. Bali kigezo kikuu ni uwezo binafsi wa mtu. Na hili lipo wazi kwa sababu kazi nyingi zinazofanyika kwenye makampuni mbalimbali, mtu yeyote anaweza kufundishwa na kufanya vizuri. Ukiondoa udaktari, sheria, uhasibu na kazi nyingine zinazohitaji leseni maalumu kuzifanya, nyingine zote mtu yeyote anaweza kufanya.
  7. Kuamini kwamba uko sahihi kwa asilimia 100 ni kikwazo kwako kupiga hatua zaidi. Na hakuna watu wanaojiamini wako sahihi kama watu ambao wanakosea. Hivyo unapaswa kuondoa dhana kwamba uko sahihi kwa asilimia 100 na kujipa nafasi ya kujifunza zaidi. Watu wengine wanapokuambia kitu ambacho hukubaliani nacho au ambacho hakiendani na unavyoamini wewe, usikikatae na kusema siyo sahihi, bali jifunze na kuona ni kwa jinsi gani kinaweza kukusaidia wewe pia. Ubishi wa kujifunza umekuwa kikwazo kwa wengi kuweza kupiga hatua zaidi kwenye maisha yao.
  8. Kuanza kidogo ni bora kuliko kutokuanza kabisa, hivyo anza sasa biashara yako pembeni na anza kwa hatua ndogo ndogo sana. Wakati sahihi kwako kuanza ni kabla hujawa na uhitaji mkubwa, kabla hujazama zaidi kwenye madeni na utumwa. Hivyo hata kama unaona ajira yako haikupi tatizo kwa sasa, usijisahau na kuona huna haja ya kujisumbua, kuna wakati utajikuta kwenye ugumu ambao njia pekee ya kutoka ni kuwa na uhuru wako. Hivyo anza kutengeneza uhuru huo sasa, hata kama haujafika hatua ya kuuhitaji sana.
  9. Swali ambalo wengi wamekuwa wanajiuliza na kukwama ni wafanye biashara gani au kitu gani cha pembeni ya ajira zao. Ukweli ni kwamba kila mtu anajua ni nini anataka kufanya, sema tu wengi hawapo tayari kuukabili ukweli huo. Kuna mawazo ambayo huwa yanajirudia rudia sana kwenye akili yako, mawazo ya kitu gani sahihi na cha muhimu kwako kufanya. Hayo ndiyo mawazo unayopaswa kuyafanyia kazi, hata kama utaanza kwa hatua ndogo sana. Hapo ulipo sasa kuna fursa nyingi zinazokuzunguka za kuyawezesha maisha yako kuwa bora zaidi. Zitumie sasa na acha kujichelewesha.
  10. Mafanikio kwenye kujiajiri yanahitaji zaidi ya kipaji. Wengi wamekuwa wanafikiri kipaji pekee kinawatosha kufanikiwa, au wengine kuamini kwa sababu hawana kipaji fulani basi hawawezi kufanikiwa. Mafanikio yoyote yanaweza kutengenezwa kupitia kupenda unachofanya, kuweka kazi sana, kuvumilia na kutokukata tamaa. Kadiri unavyoweka kazi, ndivyo wengi wanavyoamini kwamba una kipaji. Hivyo usijiambie huna kipaji, bali angalia ni kazi gani unapaswa kuweka kisha weka kazi hiyo kisawa sawa.
  11. Muda kimekua kisingizio cha wengi kushindwa kuanza kufanya kitu cha pembeni. Wengi wamekuwa wanasingizia kwamba ajira zao zinawabana na wanakosa kabisa muda. Lakini tafiti mbalimbali zinaonesha kwamba watu wanapoteza muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii na hata kuangalia tv. Hivyo kama wewe utachagua kuachana na vitu vyote vinavyochukua muda wako lakini havikulipi, utapata muda mwingi mno. Kila mtu anaweza kupata masaa mawili mpaka matano kwa siku kama akiamua kufuta kabisa yale ambayo yanampotezea muda wake. Anza sasa, kwa kuacha kufanya yale ambayo hayakuongezei kipato na utashangaa jinsi utakavyokuwa na muda mwingi.
  12. Shule imefanya kazi moja kubwa ya kutuandaa kuwa waajiriwa, hivyo unapokwenda kujiajiri jua kabisa unakwenda kinyume na msingi mzima wa elimu ulioupata. Ndiyo maana mwanzoni utakuwa na hofu kubwa, na hata wanaokuzunguka watakukatisha tamaa, siyo makosa yao, bali ndiyo msingi ambao wamejengewa. Unahitaji nguvu kubwa sana kuweza kubomoa msingi huo na kujenga msingi mpya wa kujiajiri na kupata uhuru wa maisha yako.
  13. Asilimia 99 ya biashara ndogo zinaweza kuanzishwa bila ya mtaji au kwa mtaji kidogo sana ambao mtu yeyote anaweza kuumudu kuupata kama ataamua kweli. Hivyo kinachowakwamisha watu siyo kukosa mtaji, au muda, bali kukosa utayari. Biashara nyingi ndogo unaweza kuzianzisha wewe mwenyewe kwa kutumia uzoefu wako kupitia kazi unayofanya sasa. Hilo litakuhitaji wewe kujituma zaidi, kukosa muda wa kupumzika na kutokujumuika na wengine kwenye yale ambayo umezoea. Muhimu ni kuchagua kile unachopenda kufanya na kisha kuweka nguvu zako zote kwenye kukifanya, anza na mteja mmoja, mhudumie vizuri kisha mtumie mteja huyo kupata wateja zaidi.
  14. Ili kufanikiwa kwenye safari hii ya kujiajiri ni lazima uchukue hatamu ya maisha yako na kujua kila kitu kuhusu maisha yako na kile unachofanya ni jukumu lako binafsi. Kwa maana hiyo hakuna wa kumlalamikia au kumlaumu, wewe pekee ndiye unayewajibika kwa kila kinachoendelea kwenye maisha yako. Hakuna lawama zozote unazoweza kutoa na zikakusaidia kwa namna yoyote ile. Miliki maisha yako na miliki kile unachofanya, hilo litakupa nafasi ya kupiga hatua zaidi.
  15. Unapojiajiri, unapaswa kufikiri tofauti kabisa na wale walioajiriwa. Kwa sababu kuna vitu ambavyo watu walioajiriwa hawajisumbui navyo sana, kwa sababu wameahidiwa vinafanyiwa kazi, mfano bima ya afya, mafao ya uzeeni na mengineyo. Unapoachana na ajira na kuamua kujiajiri moja kwa moja, mambo hayo utapaswa kuyahangaikia mwenyewe, lazima utafute bima yako na familia yako na pia lazima uwekeze ili kujiandaa kwa siku zijazo. Kwa sababu hakuna anayekuandalia mafao, unapaswa kutengeneza uwekezaji wako mwenyewe, ambao miaka mingi ijayo utaweza kukuingizia wewe kipato hata kama hufanyi kazi moja kwa moja.
  16. Ushindani ni mkali sana kwenye kujiajiri, kwa sababu kwa sasa ni rahisi sana kila mtu kuweza kujiajiri. Njia pekee ya kushinda kwenye mazingira haya magumu ni wewe kuwa wa tofauti na wa kipekee kwenye kile unachofanya. Usitake kuwa kama wengine, bali wewe kuwa wakipekee, kwa kutoa kile ambacho wale unaowalenga hawawezi kukipata kwa mwingine ila wewe.
  17. Unapoanza, pale ambapo bado watu wengi hawajakujua na kujua kazi zako, siyo vibaya ukaanza kwa kutoza gharama ndogo kuliko wengine wanavyotoza. Lengo ni watu wakujue na kujaribu huduma zako, na hapo unapaswa kuapa huduma bora sana zitakazowafanya warudi tena wakati mwingine na kuleta wateja wengine. Ukishatengeneza jina lako na sifa yako kwa matokeo unayozalisha, hapo sasa unaweza kuongeza bei kidogo kidogo. Utakapoanza kuongeza bei kuna wateja hawatakuelewa na wengine wataacha kupata huduma kwako, lakini jua hao siyo wateja sahihi kwako. Kazana na wale wanaoielewa thamani unayoitoa na wape thamani kubwa sana.
  18. Kwenye ajira watu wengi hutimiza majukumu yao kwa sababu wana bosi anayewafuatilia. Kwenye kujiajiri huna nafasi hiyo ya kuwa na bosi anayekufuatilia, hivyo ni rahisi sana kuzembea na kushindwa kutekeleza majukumu yako kwa muda na umakini. Hapa unahitaji kutengeneza mfumo utakaokulazimisha kutekeleza majukumu yako. Unaweza kuwa na mwenza au kikundi ambacho kwa pamoja mnasukumana kupiga hatua. Lakini pia unaweza kuwa na kocha au menta anayekusimamia kwa karibu kwenye kile unachofanya. Kutegemea wewe mwenyewe uweze kuvuka hayo ni kujipa mzigo mkubwa, tafuta watu wa kukusaidia.
  19. Unapokuwa kwenye safari hii ya kujiajiri ni rahisi sana kuridhika na mafanikio kidogo unayopata na kuanza kufanya kwa mazoea, kitu ambacho kitakurudisha nyuma au kuwapa washindani wako nafasi ya kupiga hatua kuliko wewe. Njia bora ya kuepuka hilo ni kila siku kukazana kuwa bora kuliko siku iliyopita. Kila siku mpya jisukume kupiga hatua kubwa zaidi ya zile ulizopiga kwenye siku iliyopita. Ukiweza kuishi kwa msingi huu kila siku, utakuwa unaendelea kupiga hatua zaidi kila siku. Kuwa bora leo zaidi ya jana, hilo ndilo wazo unalopaswa kuanza nalo kila siku yako.
  20. Unapofanikiwa kwenye kile unachofanya, milango mingi zaidi ya fursa inafunguka mbele yako, itumie ipasavyo. Kwa kuanzisha biashara ya pembeni na kufanikiwa sana, unapata fursa za kuwafundisha wengine nao waweze kufanya kama wewe, kuwakochi wale wanaotaka usimamizi wa karibu, kuwa mnenaji kwenye mafunzo mbalimbali, kuandika kuhusu hatua ulizochukua na wengine wakaweza kujifunza, kuendesha kozi mbalimbali na kadhalika. Hii pia inakuwa njia nzuri kwako kutoa kwa wengine pia. Hivyo unapaswa kujisukuma ufanikiwe kwenye kile cha pembeni unachofanya, kwa sababu mafanikio yako yatakaribisha fursa zaidi.

Rafiki, haya ndiyo mambo muhimu sana kujua na kufanyia kazi kutoka kwenye kitabu chetu cha juma hili, ambayo yanatuwezesha kutoka kwenye ajira na madeni na kwenda kwenye kujiajiri na uhuru wa kifedha. Umeshajifunza, sasa yaweke haya kwenye matendo na utaweza kupiga hatua sana. Usikose #MAKINIKIA ya juma hili ambapo utapata mwongozo wa kuvuka nyakati ngumu utakazokutana nazo katika safari ya kujiajiri.

#3 MAKALA YA JUMA; HATUA TANO ZA KUTOKA KWENYE AJIRA MPAKA KUJIAJIRI.

Kuna watu wapo kwenye ajira, ambazo hawazipendi na haziwalipi vizuri, na wana ndoto kubwa sana za kuondoka kwenye ajira hizo na kuwa na maisha bora sana.

Kinachoumiza ni kwamba, mipango hiyo mizuri wanayokuwa nayo huwa hawaiweki kwenye matendo. Kila mara wanaishia kuahirisha kwa kusema hawajawa tayari, hawana fedha, hawana muda, hawana uzoefu na sababu nyingine zinazoweza kuwafariji kwa muda.

Ambacho kinawakwamisha wengi ni kutokuzijua hatua za kuchukua, ambazo ni ndogo ndogo na zinamwezesha yeyote kutoka chini na kwenda juu sana.

Kwenye makala ya juma hili, tumejifunza hatua tano za kutoka kwenye ajira na utumwa mpaka kufika kwenye kujiajiri na uhuru.

Kama hukupata nafasi ya kusoma makala ya juma, unaweza kufanya hivyo hapa; Hatua Tano Za Kutoka Kwenye Ajira Usiyoipenda Na Madeni Mpaka Kufika Kwenye Kujiajiri Na Uhuru Wa Kifedha.

Endelea kutembelea mitandao ya AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA kila siku, kuna makala nzuri sana. Pia kama hupati mafunzo mazuri sana ninayotuma kwa email, fungua hapa na ujiandikishe ili kuyapokea; www.bit.ly/amkaemail

#4 TUONGEE PESA; JINSI YA KUONDOKA KWENYE MADENI YANAYOKUTESA.

Mwandishi wa kitabu cha FREELANCE TO FREEDOM aliweza kutoka kwenye madeni na kuelekea kwenye uhuru baada ya kukutana na kitabu kinachoitwa THE TOTAL MONEY MAKE OVER kilichoandikwa na Dave Ramsey.

Kwenye kitabu hicho, mwandishi anatushirikisha hatua saba za uhakika kabisa za kufikia uhuru wa kifedha au utajiri kwenye maisha yetu. Hatua hizi ni rahisi na yeyote anaweza kuzifuata, bila ya kujali anaanzia wapi. Karibu tujifunze hatua hizi saba;

Hatua ya kwanza; weka akiba ya milioni moja kama fedha ya dharura.

Hatua ya pili; lipa madeni yako yote, kasoro deni la nyumba.

Hatua ya tatu; kamilisha mfuko wako wa dharura.

Hatua ya nne; wekeza kwa ajili ya kustaafu kwako.

Hatua ya tano; lipa ada ya chuo kwa watoto wako.

Hatua ya sita; lipa deni la nyumba, au deni kubwa lingine ambalo unalo.

Hatua ya saba; TENGENEZA UTAJIRI.

Kujifunza kwa kina kuhusu hatua hizi saba za kuondoka kwenye madeni, soma hapa; UCHAMBUZI WA KITABU; THE TOTAL MONEY MAKEOVER (Mwongozo Wa Uhakika Wa Kufikia Uhuru Wa Kifedha)

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; KUPUNGUZA UHALIFU, WATU WANAPASWA KUJIAJIRI.

“How much less would we ring our hands about who will be elected next? If we collectively didn’t need their promises of better jobs—because we created those jobs—their power would diminish. Taxes would decrease. Healthcare costs would decrease, as well, because, as a society, we would be healthier. Less trips to the doctor means lower costs for everyone. Less stress means less alcohol and drug abuse. Less alcohol and drug use means less crime.” – Vincent Pugliese

Mara nyingi tumekuwa tunaweka matumaini ya maisha yetu kwa wanasiasa. Na hii ni kwa sababu tunaamini sana ahadi zao wanazotupa wakati wa kampeni kwamba watakwenda kutatua matatizo yetu yote. Watahakikisha tunapata kazi, kipato kinakuwa juu na gharama za maisha kuwa chini. Lakini kila mmoja ni shahidi kwamba ahadi za wanasiasa ni ahadi hewa, ambazo hata hao wenyewe hawajui wanawezaje kuzifikia, ila inabidi wazitoe ili washinde uchaguzi.

Njia pekee ya kila mtu kuweza kuboresha maisha yake ni kujiajiri yeye mwenyewe. Kwa sababu unapojiajiri, kipato chake kinakuwa hakina ukomo, kodi ambayo mtu analipa inapungua, gharama za matibabu zinapungua kwa sababu watu hawatakuwa wakifanya kazi wasizopenda, hivyo msongo wa mawazo unapungua na matumizi ya dawa na vilevi yanapungua. Matumizi ya dawa na vilevi yanapopungua, uhalifu unapungua.

Kwa kifupi watu wanapojiajiri na kujitengenezea kipato chao wenyewe ambacho hakina ukomo, wanasiasa wanakosa nguvu kabisa na watu wanakuwa huru.

Hivyo kama unataka uhuru kamili kwenye maisha yako, hakikisha una njia ya kuingiza kipato isiyo na ukomo.

Hizi ndizo tano za juma la 35 la mwaka huu 2019, hapa umejifunza kwa kinakuhusu kupata uhuru kamili wa maisha yako kwa kuhakikisha unakuwa na njia za kuingiza kipato zisizo na ukomo. Fanyia kazi haya uliyojifunza na hutabaki hapo ulipo sasa.

Kwenye #MAKINIKIA ya juma hili, tutakwenda kujifunza mwongozo wenye hatua saba za kuzingatia wakati wa safari yako ya kuelekea kwenye uhuru, hasa pale mambo yanapokuwa magumu. Na hatua hizi saba ni muhimu sana uzijue kwa sababu safari hii haitakuwa rahisi, utakutana na magumu mengi. Sasa unapokuwa na mwongozo sahihi, hakuna kinachoweza kukukwamisha. Pata #MAKINIKIA ya juma hili ili kuwa na mwongozo sahihi.

#MAKINIKIA haya yanapatikana kwenye channel ya TANO ZA JUMA ambayo ipo kwenye mtandao wa telegram. Kama bado hujajiunga na channel hii basi fuata maelekezo ambayo yako hapo chini.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu