Kupanga ni rahisi, kila mtu ana mipango mikubwa sana, hata kama hajui anawezaje kufikia mipango hiyo.

Kuchukua hatua ni pagumu kidogo, ndiyo maana baadhi ya wale wengi wenye mipango ndiyo wanaochukua hatua kwenye mipango waliyonayo.

Kumaliza kile ambacho mtu ameanza ni kugumu sana, ndiyo maana wachache sana kati ya wale baadhi wanaochukua hatua ndiyo wanafika mwisho wa kile walichoanza.

Wengi huacha kufanya muda mchache baada ya kuanza, pale wanapokutana na magumu au changamoto.

Hakuna mtu aliyefanikiwa kwa kuwa mtu wa kuanza na kuacha vitu, bali watu wanafanikiwa kwa kuanza kitu na kukifanya mpaka mwisho.

Jijengee nidhamu ya kumaliza kila unachoanza kufanya. Hii inakusukuma ufike mwisho wa chochote unachokuwa umeanza kufanya, na hivyo kuwa rahisi kwako kupata matokeo bora.

Na kwa kuwa mambo ya kufanya ni mengi, unapojiwekea utaratibu wa kumaliza kila unachoanza, unalazimika kuchagua vizuri kipi ufanye. Badala ya kujaribu kila kinachokuja mbele yako, unatafakari kwa kina unachotaka ni nini na kile unachotaka kufanya kinakufikishaje pale.

Kama kitu kinakupeleka kuliko bora, basi unakifanya na unakifanya mpaka mwisho bila ya kujali ni ugumu au changamoto kiasi gani utakutana nazo.

Nidhamu ya kumaliza kila unachoanza ni nidhamu itakayokufanya kuwa bora na imara na kufikia mafanikio makubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha