“Zeno always said that nothing was more unbecoming than putting on airs, especially with the young.”
—DIOGENES LAERTIUS, LIVES OF THE EMINENT PHILOSOPHERS, 7.1.22
Ni nani awezaye kusema ameiona siku hii nyingine mpya kwa sababu ya akili zake, ujanja wake na nguvu au juhudi zake?
Ni mpumbavu pekee anayeweza kufikiri hivyo.
Kuiona siku hii mpya ya leo ni bahati kwa kila mmoja wetu, kwa sababu siyo wote waliopanga kuiona siku hii wameweza kuiona.
Hivyo tunapaswa kuitumia bahati hii vizuri, ili iwe na tija kwetu na manufaa kwa wale wanaotuzunguka.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari JISHUSHE KABLA HUJASHUSHWA…
Mafanikio madogo, mara nyingi huwa ndiyo adui wa mafanikio makubwa.
Watu wengi huwa wanaanzia chini kabisa, wanakuwa na kiu ya kufanikiwa.
Kiu hiyo inawasukuma kujifunza sana, kujituma sana, kuwa na nidhamu kubwa kwenye fedha, muda na hata mambo binafsi.
Kwa kuanza na hayo, mambo yanaanza kubadilika na mtu anaanza kupata mafahikio kidogo.
Hapo sasa ndipo mambo yanaanza kuharibika,
Kwa kupata mafanikio kidogo mtu anajiona ndiyo ameshamaliza kila kitu,
Anaona ameshajua kila kitu hivyo hana haja ya kujifunza tena.
Anaona ameshaweka juhudi sana hivyo hana haja ya kujitesa tena na kazi.
Anaona ameshapiga hatua hivyo hahitaji tena zile nidhamu za kujinyima alizokuwa amejijengea.
Na hapa ndipo anguko linapotengenezwa na kutokea.
Baada ya mtu kuwa amejikweza sana, kinachofuata ni kuangushwa.
Kama tunataka kufikia mafanikio makubwa kuliko tuliyonayo sasa,
Kama tunataka kudumu kwenye mafanikio makubwa kwa maisha yetu yote,
Basi tunapaswa kujishusha kila wakati,
Tunapaswa kujua kwamba kujifunza hakuna mwisho, haijalishi tumefika wapi.
Tunapaswa kujua kuweka kazi hakuna mwisho, kadiri tunavyofanikiwa ndivyo tunavyopaswa kujituma zaidi.
Tunapaswa kujua nidhamu haina kutosheka, kila wakati tunapaswa kuendeleza nidhamu zetu.
Kwa asili kila kinachokwenda juu huwa kinavutwa kurudi chini,
Inahitaji kazi kuzuia nguvu hii inayorudisha vitu chini,
Na ili kuepuka kushushwa chini na dunia, anza kujishusha wewe mwenyewe kwanza.
Ukishakuwa chini, hakuna kinachoweza kukushusha tena chini.
Unapojipaisha angani, dunia inafurahi sana kukushusha chini.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujishusha na kuepuka kujikweza bila ya kujali mafanikio kiasi gani umefikia.
#KinachojikwezaHuangushwa #KuwaMnyenyekevu #UnapofikiriUnajuaKilaKituNdiyoHujuiChochote
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1