Watu huwa wanalalamika kwamba biashara ni ngumu, lakini wamekuwa hawajui kwa uhakika ugumu wa biashara hizo uko wapi na hivyo kushindwa kujua hatua sahihi za kuchukua ili kuvuka ugumu huo. Kwa kutokujua ugumu hasa ulipo, wengi wamekuwa wanashindwa kwenye biashara.
Kutengeneza kitu ambacho unauza kwenye biashara yako siyo kugumu, ukishajua kutengeneza unaweza hata kuwafundisha wengine nao wakatengeneza. Hivi unafikiri kuna ugumu gani kwenye kutengeneza maandazi, karanga na hata vitu vingine? Kila mtu anayejifunza kwa muda anaweza kutengeneza vizuri.
Kununua vitu kwa bei ya jumla kwa gharama za chini kidogo na kwenda kuviuza kwa bei ya reja reja ambayo inakuwa juu ya ile ya kununulia siyo kugumu. Nani asiyejua kwamba akienda duka la jumla anaweza kununua viatu kwa shilingi elfu tatu na akifika kwa watu akawauzia elfu 5, kila mtu anajua hilo, hakuna ugumu wowote hapo.
Ugumu hasa kwenye biashara uko kwenye kuwashawishi watu watoe fedha zao, watu wakupe wewe fedha zao ambazo wamezitafuta kwa shida na wana matumizi mengine muhimu ya fedha hizo na tena hazitoshelezi. Ugumu ni wewe kuweza kuwa na ushawishi wa kutosha kwa watu hao kuona kwamba kile unachouza wanakihitaji na wanakihitaji sasa.
Kwa maneno mengine, ugumu wa biashara yoyote ile upo kwenye mauzo. Hakuna zaidi ya hapo, vitu vingine vyote kwenye biashara ni rahisi kufanya na ukiwaelekeza watu vizuri wanaweza kufanya. Ni kwenye mauzo ambapo kunahitaji sayansi, sanaa, saikolojia na mahusiano mazuri mpaka mteja akuelewe na kukupa fedha yake aliyoipata kwa taaabu.
Kazi ngumu kwenye biashara ni kupata umakini wa watu na watu hao kukuamini wewe. Ugumu upo kwenye kuwasaidia watu kufanya maamuzi sahihi ambayo hawatayajutia baadaye. Ugumu upo kwenye kutengeneza mahusiano bora na wateja wako.
Kuvuka ugumu huu inakuhitaji muda wa kutengeneza mahusiano bora na wateja wako, kuchagua wateja ambao unawalenga, kujua matatizo na mahitaji yao makubwa na kisha wewe kuwa mshauri wao kwenye maeneo hayo. Usiishie tu kuwa muuzaji, kuwa mshauri unayeweza kutegemewa na watu watakuwa tayari kununua kwako. Na hapa ni kama unataka kujenga biashara itakayodumu kwa muda mrefu.
Weka juhudi zako kwenye kujifunza mauzo, ushawishi na hata namna bora ya kutengeneza mahusiano na wateja wako na hilo litakuwezesha kufanikiwa kwenye biashara yoyote ile utakayochagua kufanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,