Tunaishi kwenye zama ambazo umaarufu unatukuzwa sana.

Na hii ni kwa sababu katika zama hizi, umaarufu ni rahisi kupatikana na yeyote anaweza kuwa maarufu kwa wakati wowote ule. Uwepo wa mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii imerahisisha sana hilo la watu kutafuta umaarufu.

Na watu wamekuwa wanafanya mambo ya hovyo na yanayoharibu sifa zao kwa kutaka kupata umaarufu. Mfano kuweka picha zao za uchi mitandaoni, kuweka mada chonganishi mitandaoni na kadhalika.

Kwenye upande wa biashara hili pia limeshamiri, watu wengi wanakazana kujenga umaarufu badala ya kujenga biashara imara. Watu wengi wanataka kujulikana na kila mtu badala ya kujulikana na watu sahihi.

Wengi wanaoingia kwenye biashara wamekuwa wanaingia kwa dhana kwamba wakijulikana na kila mtu basi biashara yao itakuwa. Hivyo wanatumia muda na gharama kubwa kujitangaza ili kujulikana na kila mtu.

Kwa zama hizi tunazoishi sasa, zama zenye kelele nyingi, zama zenye ushindani mkali, wateja hawafanyi tena maamuzi ya manunuzi kwa kigezo cha umaarufu. Badala yake wanafanya maamuzi kwa kigezo cha uaminifu. Watu wananunua kwa watu ambao wanawaamini. Kwa sababu siku hizi kila mtu anaweza kuahidi, halafu asitimize ahadi yake.

Wateja wameshaumizwa sana kiasi kwamba wamejifunza wale wanaoweka nguvu nyingi kwenye umaarufu siyo ambao wanaweka nguvu nyingi kwenye kuwahudumia.

Hivyo na wewe badili mkakati, badala ya kuweka lengo la kutafuta umaarufu, weka lengo la kutengeneza uaminifu kwa wale unaowalenga. Kwa hakika watakuwa wachache, lakini watakuwa wenye maana na mchango mkubwa kwako kuliko kuwalenga wengi kwenye umaarufu.

Uaminifu unalipa kuliko umaarufu, uaminifu unakupa utulivu mkubwa kuliko umaarufu. Uaminifu unajenga mahusiano bora kuliko umaarufu.

Kama unataka kujenga biashara imara, itakayodumu kwa muda mrefu na kukupa mafanikio, peleka nguvu zako kwenye kujenga uaminifu na siyo umaarufu. Jenga mahusiano bora na wateja wako kwa kujitoa kweli kuhakikisha wanapata kilicho sahihi kwao, unatatua matatizo yao na kutimiza mahitaji yao.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha