Mpendwa rafiki yangu,
Miongoni mwa viumbe vinavyokataa tamaa hapa duniani ni binadamu, licha ya kupewa uwezo mkubwa wa kiakili wa kutambua zuri au baya lakini bado unakuta mtu anakata tamaa na hata kuahirisha kile alichopanga kufanya yeye mwenyewe. Huwa tunajidharau sisi wenyewe pale tunapopanga halafu tunashindwa kutekeleza kile tulichopanga.
Watu wanataka mambo yao yaende kama vile wanavyotaka wao, hawapendi kusikia changamoto kwenye kile wanachofanya na wakiona wanakutana na changamoto wanahisi kama vile dunia imemuona kwanini yeye na siyo wengine.
Unapofanya kitu chochote tegemea kukutana na upinzani, ni kawaida ya dunia kutupinga kwa mfano, hata wewe ukichukua jiwe na kurusha juu lazima litarudisha haraka chini. Hivyo nguvu iliyoko ya kuturudisha chini ni kubwa ili usimame unahitaji uweke kazi kweli.
Kama umefikia mahali na umeona umeshindwa kabisa hata kupiga hatua basi leo ninakwenda kukutoa hapo ulipo kwenye huo mkwamo kupitia makala hii.
Kama umejiona umeshindwa kwenye kile unachofanya jiulize je umeshindwa mara ngapi? Kama umeshindwa mara moja, mbili kumi au mara ngapi?
Kama umeshindwa mara mia moja bado hujashindwa endelea kujaribu kwa sababu aliyegundua taa Thomas Edison alishindwa zaidi ya mara elfu kumi sasa iweje wewe useme umeshindwa kwa kufanya mara moja? Mbili au tatu?
Siyo kwamba umeshindwa, bali hujajaribu vya kutosha kwenye kile unachofanya. Changamoto ya watu wengi ni kwamba hawapendi shida, wakisumbuliwa kidogo tu wanaamua kuacha kile wanachofanya na kurudi kwenye mazoea.
SOMA; Hii Ndiyo Njia Pekee Ya Kutoka Hapo Ulipokwama Sasa Hivi Na Kufanikiwa Zaidi.
Rafiki, kama Thomas alivyokuwa king’ang’anizi ndivyo na wewe unatakiwa kuwa king’ang’anizi mpaka upate kile unachotaka. Usiseme umeshindwa bali jaribu vya kutosha kwa kuwa mbishi.
Dunia huwa haitoi ushindi kirahisi, ni mpaka pale utakapokuwa king’ang’anizi kweli ndiyo itaamua kukupa kile unachotaka.
Hatua ya kuchukua leo; usiseme umeshindwa bali unatakiwa kujaribu zaidi ya hapo ulipokwama, unapojiona umejaribu na kushindwa jiulize je umejaribu kama Thomas zaidi ya mara elfu 10? Kama ni hapa bado hujashindwa endelea kuweka kazi.
Makala hii imeandikwa na
Mwl. Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa http://kessydeo.home.blog vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI. Karibu sana.
Ukawe na siku bora sana rafiki.
Rafiki na mwalimu wako,
Mwl, Deogratius kessy
0717101505/0767101504
deokessy.dk@gmail.com //kessydeoblog@gmail.com
Asante sana