“Show me someone who isn’t a slave! One is a slave to lust, another to greed, another to power, and all are slaves to fear. I could name a former Consul who is a slave to a little old woman, a millionaire who is the slave of the cleaning woman. . . . No servitude is more abject than the self-imposed.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 47.17
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii bora ambayo tumeiona leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari HATARI YA UTEGEMEZI…
Kila mmoja wetu ana utegemezi, ulevi au uraibu ambao tayari ameshajijengea.
Kuna vitu ambavyo umeshavizoea sana na unavitegemea sana kiasi kwamba unajiambia maisha yako hayawezi kwenda bila ya vitu hivyo.
Tunaweza kuchukulia hili kirahisi, lakini tunakuwa tumechagua kuwa watumwa sisi wenyewe.
Chochote unachojiambia huwezi kuishi bila ya kuwa nacho, kinakufanya wewe uwe mtumwa.
Na kwa kuwa tunajua tunaweza kupoteza chochote tulichonacho, tunakuwa tumejiweka kwenye nafasi ya kuumizwa na kuvurugwa pale kile tunachotegemea sana kinapoondoka au kuondolewa.
Kama unataka kuwa huru wakati wote,
Kama unataka kuwa na maisha tulivu na yasiyovurugwa, basi hakikisha hakuna kitu chochote unachoweka mategemeo yako yote.
Haimaanishi kwamba huhitaji chochote, bali huweki mategemeo yako yote kwenye kitu chochote.
Ukiwa nacho unakitumia kwa usahihi, usipokuwa nacho hujutii wala maisha yako hayavurugiki.
Ili kuweza kutifikia hatua hiyo ya uhuru na utulivu wa kutotegemea chochote moja kwa moja, unapaswa kujipa zoezi la kutokutegemea kile ambacho umeshajijengea mazoea sana.
Yaani jifunze kuacha kufanya au kutumia kitu hata kama unacho au unaweza kufanya hivyo.
Kama umezoea kula chakula fulani au kunywa kinywaji fulani, hebu chagua kuacha kula au kunywa kwa kipindi fulani, hata kama ipo ndani ya uwezo wako kupata vitu hivyo.
Zoezi kama hili linakuimarisha na kuondoa utegemezi wako, siku unapokosa kabisa, haikuvurugi.
Fanya zoezi hilo kwenye kila kitu ambacho unajiambia huwezi kuishi bila ya kuwa nacho. Tengeneza mfungo kwenye kila kitu cha aina hiyo, siku, wiki au hata miezi ambayo utaenda bila ya kutegemea vitu hivyo na hilo litakufanya kuwa imara zaidi.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuondoa utegemezi, ulevi na uteja kwa kitu chochote kilicho nje yako ili uweze kuwa huru na mwenye utulivu wakato wote.
#UsiwekeMategemeoKwaVituVyaNje #TunzaUhuruNaUtulivuWako #FungaKwaKileUlichozoea
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1