Kila mmoja wetu anapitia magumu na changamoto mbalimbali kwenye maisha yake.

Lakini tukiwaangalia watu kwa nje, kuna ambao tunawaona wana magumu zaidi ya wengine, na kuna ambao tunaona wao wana afadhali.

Lakini unaporudi kuangalia kwa ndani, unagundua wote wana magumu na changamoto sawa, ila wale wanaoonekana changamoto zao ni kubwa zaidi, ni kwa sababu wamechagua kuzikuza zaidi ya zilivyokuwa. Na wale ambao wanaonekana changamoto zao ni ndogo, ni kwa sababu wamechagua kutokuzikuza zaidi.

Ni kawaida yetu sisi binadamu kuhamaki na kuchukua hatua za haraka pale tunapokutana na ugumu au changamoto ambazo hatukuzitegemea. Tunayafanya mambo kuwa magumu kuliko yalivyo. Tunafanya hivyo kwa kulalamika, kulaumu wengine, kukasirika, kukata tamaa na kuamua kuacha. Wakati mwingine tunakazana kubadili kile ambacho kimeshatokea, na hapo tunazidi kuharibu zaidi. Au kutafuta njia ya kuficha kile kilichotokea au kuepuka madhara ya matokeo yake.

Hatua zote hizi tunazokazana kuchukua kukabiliana na magumu au changamoto tunazokutana nazo, ni kama zinaogeza mafuta ya taa kwenye moto ambao tayari unawaka, zinachochea tatizo kuwa kubwa zaidi.

Kuepuka hali hii ya kukuza changamoto na magumu tunayopitia, hatua ya kwanza ni kutokufanya chochote, kujipa muda wa kufikiri na kutafakari kwa kina nini kimetokea na umechangiaje kwenye kile kilichotokea. Na hapo utaweza kuona vizuri changamoto hiyo na hatua sahihi za kuchukua kuitatua.

Mara nyingi changamoto unazopitia hazikuhitaji wewe ufanye chochote, unapaswa kuzipa muda tu na zitapotea zenyewe au utazizoea na kusonga mbele.

Usipoteze nguvu zako kujaribu kukwepa, kuficha au kubadili chochote ulichofanya na kuzalisha changamoto kwenye maisha yako. Badala yake fikiri kwa kina na chukua hatua sahihi, kama hujapata hatua sahihi za kuchukua subiri. Muda huwa ni tiba sahihi kwa changamoto yoyote inayokusumbua.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha