Tabia moja tuliyonayo sisi binadamu ni kupenda kuonekana tunajua kitu ambacho wengine hawajui, na tunapopata nafasi ya kueleza kitu hicho, basi tunahakikisha tumeonesha kwamba tunajua kile ambacho wengine hawajui.

Na tabia hii imekuwa na madhara makubwa kwa wengi, japo wale wanaoifanya wamekuwa hawajui madhara wanayosababisha kwa wengine.

Zipo njia mbili ambazo watu huweza kuonesha kile wanachokijua zaidi, njia hizo ni maoni na ushauri.

Kwenye maoni mtu anaonesha ujuzi wa juu na usahihi wake yeye na makosa anayofanya mwingine. Kwenye ushauri, mtu anaonesha ujuzi wake kwa namba ambavyo unaweza kumsaidia mtu mwingine.

Hivyo maoni yana lengo la kukosoa, wakati ushauri una lengo la kusaidia.

Hivyo kama unataka wengine wakupe mchango wao wa mawazo juu ya kile unachofanya, ni vyema ukaomba ushauri na siyo maoni. Unapoomba maoni unawapa watu uwanja wa kukukosoa na kukukatisha tamaa. Unapoomba ushauri unawapa watu nafasi ya kukusaidia zaidi.

Chukua mfano unataka kuanzisha au umeanzisha biashara fulani, na unataka kusikia kwa wengine wana kipi cha kukuambia kuhusu biashara hiyo.

Kama utaomba maoni, moja kwa moja watu wanakwenda upande wa kukosoa au kuonesha kwa nini ni ngumu, haiwezekani au itashindwa. Kwenye maoni watu huwa wanakuwa na msimamo mkali kwenye kile wanachoamini wao, hata kama siyo sahihi.

Kwa upande wa pili, kama utaomba ushauri, kumwomba mtu akushauri ni namna gani unaweza kufanya vizuri zaidi au kufanikiwa, mchango utakaoupata utakuwa wa tofauti kabisa. Watu watakupa mchango bora sana wa namna bora ya kufanikiwa kwenye kitu hicho, watapenda sana kuona wamechangia kwenye mafanikio yao kupitia ushauri wako.

Ni watu wachache sana ambao utawaomba maoni yao na wakakupa mchango ambao unakupa moyo wa kuendelea, wengi wataweka maelezo yanayokatisha tamaa au kukujaza hofu. Na kadiri mtu anavyokuwa na misimamo mikali, ndivyo maoni yake yanavyokuwa mabaya.

Ni watu wachache sana ambao utawaomba ushauri na kuanza kukuambia huwezi au haiwezekani. Kwa asili watu wanapenda kusaidia pale wanapoombwa, hivyo unapoomba ushauri, moja kwa moja watu wanaenda kukupa mchango ambao utakusaidia.

Tuangalie mfano mwingine unaounga mkono utayari wa watu kukusaidia. Angalia mara zote unapokuwa unaenda mahali usipojua na kuwauliza watu wakuelekeze, wataacha kila wanachofanya na kukuelekeza kwa usahihi, tena kuhakikisha umeelewa, hata kama hawakujui. Ni watu ambao huwajui na wala hawakujui, umewakatisha kwenye chochote wanachofanya na kuwaomba wakuelekeze kule unakotaka kufika na hupajui, na watakuwa tayari kukusaidia kwenye hilo.

Omba ushauri, usiombe maoni, ushauri unajenga, maoni yanabomoa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha