“So someone’s good at taking down an opponent, but that doesn’t make them more community-minded, or modest, or well-prepared for any circumstance, or more tolerant of the faults of others.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 7.52
Ni siku nyingine mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Tumepata fursa nyingine ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KUWA MTU BORA NA SIYO KUWA NA VITU BORA…
Juhudi kubwa unazoweka kwenye maisha yako, lengo lake ni nini?
Unapofanya kazi usiku na mchana, unasukumwa na kitu gani?
Kuna misukumo ya aina mbili kwenye kila tunachofanya.
Msukumo wa kwanza ni kuwa mtu bora, hapa unakazana wewe kuwa bora zaidi leo kuliko ulivyokuwa jana. Msukumo huu ndiyo unakufanya ukue zaidi wewe kama mtu na uweze kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha.
Msukomo wa pili ni kuwa na vitu bora, hapa unakazana kupata vitu vizuri, vitakavyoonesha kwamba wewe ni zaidi ya wengine. Msukumo huu unakuweka kwenye mashindano na wengine, unakufanya uonekane ni bora kwa nje, japo ndani unakuwa siyo bora. Msukumo huu unakufanya utumie nguvu nyingi kuwaonesha wengine vitu fulani, wakati ndani yako bado kuna utupu. Na tatizo kubwa la kutaka kuwa bora kwenye vitu, huwa kila wakati kuna kitu bora kuliko kile ulichonacho.
Turudi kwako, ujiulize na kutafakari tena kwa kina, ni msukumo gani unaokufanya wewe ujitume zaidi?
Kama ni wewe kuwa bora upo kwenye njia nzuri na utafanikiwa sana.
Lakini kama ni wa kupata vitu vilivyo bora, upo kwenye njia ya kupotea na japo kwa nje unaweza kuonekana umefanikiwa, ndani yako kutakuwa na utupu mkubwa.
Hakikisha una msukumo sahihi, msukumo wa kutaka kuwa bora zaidi wewe kama mtu na siyo kutaka kupata vitu bora zaidi. Ukianza na kuwa bora zaidi wewe, unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kupata vile vilivyo bora zaidi.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kukazana kuwa bora zaidi wewe na siku kukazana kupata kilicho bora zaidi.
#KazanaKuwaBora #UsishindaneNaWengine #UkiwaBoraUtafanyaMakubwa
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1
Asante kocha kwa hili, nitajitahid kuwa bora natambua nikiwa bora na vitu bora vitatokea pia kwenye maisha yangu
LikeLike
Vizuri James.
LikeLike