Unafikiri ni kitu gani kinapelekea mtu kucheza bahati nasibu ya shilingi mia tano au elfu moja?

Wachezaji wengi wa bahati nasibu hizi wanajua kabisa kwamba hawawezi kushinda, kwa sababu washindi ni wachache na wachezaji ni wengi.

Lakini kinachowasukuma kucheza bahati nasibu hizi ni yale matumaini wanayokuwa nayo kwamba huenda nao wakashinda. Hawana uhakika wa kushinda, lakini kwa kushiriki, wanakuwa na matumaini kwamba huenda watashinda.

Na kwa kuwa kiwango wanacholipa ili kushiriki bahati nasibu hizi ni kidogo, kama mia tano au elfu moja, kinakuwa na thamani sahihi kwa matumaini wanayoyapata baada ya kushiriki na kabla ya kushindwa.

Hivyo mchezaji wa bahati nasibu, anakuwa na matumaini makubwa baada ya kununua tiketi ya bahati nasibu kwamba huenda akashinda. Utafiti umewahi kufanyika, ambapo watu walionunua tiketi ya kushiriki bahati nasibu walipewa mara kumi ya kiasi walicholipa ili wauze tiketi zao kabla ya bahati nasibu, na asilimia kubwa hawakuwa tayari kufanya hivyo.

Kwa mfano mtu amenunua tiketi ya bahati nasibu kwa shilingi elfu moja, anapewa nafasi ya kuuza tiketi hiyo kwa shilingi elfu kumi kabla ya bahati nasibu, lakini anakataa. Kinachomfanya mtu akatae mara kumi ya kile alichowekeza ni matumaini kwamba anaweza kupata zaidi.

Lakini matumaini haya ya wacheza bahati nasibu huwa yanapotea pale bahati nasibu inapochezeshwa na wakashindwa. Ila huwa wanayapata upya kwa kununua tena tiketi. Na hilo limekuwa linachangia kwenye ulevi wa bahati nasibu ambao wengi wamekuwa wanaingia. Siyo kwa sababu hawawezi kuona ufinyu wa nafasi ya wao kushinda, ila kwa sababu ya matumaini wanayoyapata kwa kununua ushiriki kwenye bahati nasibu hizo.

Unachopaswa kujifunza hapa ni kimoja, watu wapo tayari kulipa zaidi kwa matumaini, je kwenye biashara yako ni matumaini gani unayouza? Angalia hata kwenye biashara za vitu vya starehe na kifahari, kinachouzwa siyo kile kitu halisi, bali yale matumaini ambayo watu wanakuwa nayo.

Japokuwa matumaini siyo mkakati, lakini hakikisha kwenye biashara yako kuna matumaini ambayo unamuuzia mteja wako. Hakikisha kuna picha ambayo mteja wako anaipata, kwa namna maisha yake yatabadilika na kuwa bora kutokana na yeye kununua kile ambacho unakiuza. Hata kama siyo kitakachotokea kwa uhakika, yale matumaini unayojenga yanawasukuma watu kuchukua hatua.

Unapaswa kuwa makini sana kwenye hili, kwa sababu hapa ndipo wengi hujikuta wanadanganya na kulaghai, kitu ambacho kinaleta madhara kwenye biashara zao. Wape wateja wako matumaini sahihi na watakuwa tayari kwenda na wewe kwa muda mrefu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha