Unafikiri ni kitu gani kinapelekea mtu kucheza bahati nasibu ya shilingi mia tano au elfu moja?
Wachezaji wengi wa bahati nasibu hizi wanajua kabisa kwamba hawawezi kushinda, kwa sababu washindi ni wachache na wachezaji ni wengi.
Lakini kinachowasukuma kucheza bahati nasibu hizi ni yale matumaini wanayokuwa nayo kwamba huenda nao wakashinda. Hawana uhakika wa kushinda, lakini kwa kushiriki, wanakuwa na matumaini kwamba huenda watashinda.
Na kwa kuwa kiwango wanacholipa ili kushiriki bahati nasibu hizi ni kidogo, kama mia tano au elfu moja, kinakuwa na thamani sahihi kwa matumaini wanayoyapata baada ya kushiriki na kabla ya kushindwa.
Hivyo mchezaji wa bahati nasibu, anakuwa na matumaini makubwa baada ya kununua tiketi ya bahati nasibu kwamba huenda akashinda. Utafiti umewahi kufanyika, ambapo watu walionunua tiketi ya kushiriki bahati nasibu walipewa mara kumi ya kiasi walicholipa ili wauze tiketi zao kabla ya bahati nasibu, na asilimia kubwa hawakuwa tayari kufanya hivyo.
Kwa mfano mtu amenunua tiketi ya bahati nasibu kwa shilingi elfu moja, anapewa nafasi ya kuuza tiketi hiyo kwa shilingi elfu kumi kabla ya bahati nasibu, lakini anakataa. Kinachomfanya mtu akatae mara kumi ya kile alichowekeza ni matumaini kwamba anaweza kupata zaidi.
Lakini matumaini haya ya wacheza bahati nasibu huwa yanapotea pale bahati nasibu inapochezeshwa na wakashindwa. Ila huwa wanayapata upya kwa kununua tena tiketi. Na hilo limekuwa linachangia kwenye ulevi wa bahati nasibu ambao wengi wamekuwa wanaingia. Siyo kwa sababu hawawezi kuona ufinyu wa nafasi ya wao kushinda, ila kwa sababu ya matumaini wanayoyapata kwa kununua ushiriki kwenye bahati nasibu hizo.
Unachopaswa kujifunza hapa ni kimoja, watu wapo tayari kulipa zaidi kwa matumaini, je kwenye biashara yako ni matumaini gani unayouza? Angalia hata kwenye biashara za vitu vya starehe na kifahari, kinachouzwa siyo kile kitu halisi, bali yale matumaini ambayo watu wanakuwa nayo.
Japokuwa matumaini siyo mkakati, lakini hakikisha kwenye biashara yako kuna matumaini ambayo unamuuzia mteja wako. Hakikisha kuna picha ambayo mteja wako anaipata, kwa namna maisha yake yatabadilika na kuwa bora kutokana na yeye kununua kile ambacho unakiuza. Hata kama siyo kitakachotokea kwa uhakika, yale matumaini unayojenga yanawasukuma watu kuchukua hatua.
Unapaswa kuwa makini sana kwenye hili, kwa sababu hapa ndipo wengi hujikuta wanadanganya na kulaghai, kitu ambacho kinaleta madhara kwenye biashara zao. Wape wateja wako matumaini sahihi na watakuwa tayari kwenda na wewe kwa muda mrefu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ahsante sana Kocha,
Kuna makala nilisoma kupitia tafsiri za Wikpedia ilisema
Michezo yote ya bahati na sibu haipo kwaajili ya kutengeneza ushindi wa mchezaji bali kutengeneza ushindi wa mchezeshaji,
Unauhakika wa kushiriki michezo hiyo kila siku na kila wakati uwezavyo lakini hauna uhakika wa kushinda kila siku wala kila muda.
Anasema iwapo kumachochote kinafanyika kwa kukuahidi kupata fedha nyingi kuliko kiwango ulicho wekeza wala hakuna maarifa yoyote unayo paswa kuwa nayo ili kupata kiwango hicho cha fedha basi shituka haraka sana.
Kwenye Makala nyingine kupitia Jamii Forum yupo kijana wa kitanzania alie elezea safari yake ya kuingia kwenye michezo hii,
Alieleza namna ilivyo sambaratisha familia yake,Alieleza namna ilivyo mwingiza kwenye Ulevi na matumizi ya pombe akiamini anapunguza mawazo,Alieleza namna ilivyo mfilisi biashara yake,Alieleza namna anavyo shindwa kuacha leo akiamini kesho yaja atashinda lakini hilo halijawai kutokea,
Anasema amepoteza zaidi Ya Ml 30 kwenye kamali huku fedha alizo shinda si zaidi ya Ml 5 na hii ni ule ushindi mdogo mdogo tu,Anasema kwenye kipindi chote amekuwa akijilipua kwa kucheza michezo yenye dau kubwa huku akijiambia iwapo atashindwa ni hasara na kama atashinda basi iwe ametoboa mazima lakini hilo limesalia kuwa ndoto.
KAA MBALI NA MICHEZO YA BAHATI NA SIBU.
KAA KARIBU NA KUIPENDA KAZI DAIMA.
LikeLike
Asante Ernest kwa kutushirikisha madhara haya makubwa ya michezo ya bahati nasibu. Ubaya mkubwa ni uraibu ambao michezo hii inatengeneza, mtu akishaingia, ni vigumu sana kutoka.
LikeLike
Shukrani Sana kocha hii ni Siri nzito mno. Kweli kabisa watu huwa tunanunua matumaini ambayo tunapewa kutoka Kwa wale wanaotuuzia Huduma au bidhaa.
LikeLike
Karibu Tumaini.
LikeLike