Kwa asili, sisi binadamu ni viumbe wabinafsi.

Huwa tunaweka maslahi yetu mbele kabla ya maslahi ya watu wengine.

Na hili halina ubaya wowote, kwa sababu ndiyo limetuwezesha kuendelea kuwa hai na kuzaliana.

Chochote tunachofanya, huwa tunaanza kujiuliza kinatusaidia nini sisi kwanza. Au kuna manufaa gani yaliyopo kwa ajili yetu.

Kujua hili ni muhimu sana kwako, kwa sababu kila mara utahitaji kuwashawishi watu wengine wakubaliane na wewe.

Iwe ni kitu unauza na unataka wengine wakubali kununua, iwe ni hoja unazo na unataka wengine wakubaliane nazo na hali nyingine kama hizo.

Chochote unachotaka mwingine akubaliane na wewe, mwoneshe ni jinsi gani kitamnufaisha yeye, inaweza kuwa sasa au baadaye, lakini muhimu ni mtu ayaone wazi manufaa atakayopata kwa kuchukua hatua unayomshawishi achukue.

Kwa kila hatua ambayo mtu anachukua, kuna hali ya kupata au kupoteza. Ni vigumu sana kufanya maamuzi hayo kama huna kitu kizuri na kikubwa unachotegemea kupata.

Wasaidie wale unaowashawishi waweze kufanya maamuzi kwa kuwaonesha manufaa wanayokwenda kupata kwa kufanya maamuzi hayo.

Kama unauza, usitumie muda mwingi kumweleza mtu sifa za kile unachomuuzia, bali tumia muda huo kumweleza jinsi gani kitu hicho kitakuwa na manufaa kwake. Ni kitu kidogo ambacho ukikibadili utaweza kuongeza zaidi mauzo yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha