Hofu ndiyo kikwazo kwa wengi kuchukua hatua ambazo wanajua wanapaswa kuchukua ili kufanikiwa.

Na moja ya hofu ambayo imekuwa kikwazo kwa wengi ni hofu ya kushindwa.

Sote tunajua kwamba kama tunataka kufanikiwa tunapaswa kufanya kitu cha tofauti, tunapaswa kuchukua hatua ambazo hatujawahi kuchukua huko nyuma.

Lakini hatua hizo za tofauti zina hatari, hatari ya kushindwa, kwa sababu hatujawahi kufanya hivyo tena, hivyo hatuna uhakika.

Sasa wengi wanapoifikiria hatari hiyo ya kushindwa, huona ni bora wasifanye kitu hicho.

Lakini kutokufanya hakuleti unafuu, badala yake ndiyo kunazidi kukupa mzigo mkubwa kwenye maisha yako.

Kushindwa ni mara moja, kama utafanya kitu na kushindwa, utashindwa mara moja na kupitia kushindwa huko utajifunza njia sahihi ya kupita au njia isiyo sahihi ya kuepuka.

Majuto ni milele, kama kuna kitu unataka kufanya, lakini ukaamua usifanye, kila mara utajutia hali hiyo ya wewe kutokuchukua hatua. Kila wakati utafikiria kama ungechukua hatua huenda ungepata matokeo ya tofauti. Majuto haya yatakuwa mzigo mzito kwako na yatakusumbua sana kuliko kufanya na kushindwa.

Hivyo rafiki, kuondokana na hali ya majuto ambayo yatakusumbua sana, kuwa mtu wa kuchukua hatua, kuwa mtu wa kujaribu vitu vipya na kama utashindwa basi utajifunza. Usikubali kubeba majuto maisha yako yote, unapokuwa na kitu ambacho unaona unapaswa kufanya, kifanye, hata kama kuna hofu ya kushindwa. Ni bora ufanye na kushindwa kuliko kutokufanya na kubeba majuto maisha yako yote.

Kuwa mtu wa kufanya, usiwe mtu wa kubeba majuto.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha